CCM YAIAGIZA SERIKALI KUNUNUA TANI 100,000 ZA MAHINDI KUKABILIANA NA UHABA WA CHAKULA MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Monday, September 6, 2021

CCM YAIAGIZA SERIKALI KUNUNUA TANI 100,000 ZA MAHINDI KUKABILIANA NA UHABA WA CHAKULA MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI


Katibu Mkuu wa CCM,Daniel Chongolo
Katibu Mkuu wa CCM,Daniel Chongolo

Na Dotto Kwilasa, Dodoma.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua tani 100,000 za mahindi katika Mikoa ya Nyanda za juu Kusini kuondokana na Uhaba wa chakula.

Hatua hii imekuja wakati ambapo tayari Serikali imekwishanunua tani 24,000 kiasi ambacho kimeelezwa kuwa ni kidogo na kwamba hakiwezi kukidhi mahitaji ya wananchi.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 6,2021,na Katibu Mkuu wa CCM,Daniel Chongolo wakati akiongea na Waandishi wa habari huku akifafanua kuwa Mwezi Julai Sekretarieti ya Chama hicho ilifanya ziara katika Mikoa ya Rukwa,Songwe na Mbeya ambapo walikutana na changamoto ya wakulima kukosa soko la zao la mahindi.

Amesema mara baada ya ziara hiyo waliiagiza Serikali kununua mahindi hayo ambapo ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 14 ambazo zilinunua zaidi ya tani 24,000.

Amedai kwa sasa fedha hizo zimeisha na wakulima wanaendelea kuhangaika kutafuta soko la kuuzia mahindi yao.

Kutokana na hali hiyo Katibu Mkuu huyo ameiagiza Serikali kutoa tena fedha na inunue tani 100,000 za wakulima hao kwani wanazotaarifa kwamba msimu ujao wa kilimo mvua zitakuwa chache.

“Tena kwa bei ile ile ya shilingi 500 kwa kilogramu na wafanye zoezi hilo liwe endelevu kwani mamkala ya hali ya hewa imesema kuna changamoto katika mvua za vuli mpaka katika mvua za masika hivyo kutakuwa na changamoto ya upatikanaji wa chakula,”amesema.

Pia amesema katika ziara hiyo wamejifunza kwamba uchache wa vituo vya kununulia mahindi hivyo ameiagiza NFRA kuweka vituo ambavyo vitakuwa karibu na wakukulima.

“Kuna malalamiko kukatwa fedha katika shilingi 500 tunasema hapana mtu aliyepo Mufindi,Ileje,Mbozi,Nkasi tunataka bei ya mahindi iwe moja kwa wote wa karibu na mbali,”amesema Chongolo.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo ameziagiza Wizara za Kilimo na Fedha na Mipango wakutane kujadiliana jinsi ya kupunguza bei ya mbolea kutokana na kuwa juu hivyo kumuumiza mkulima.

Amesema kwa sasa bei ya mbolea aina ya Urea imepanda maradufu kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona ambapo awali ilikuwa shilingi 50,000 mpaka 55,000 lakini kwa sasa ni shilingi 80,000 mpaka 85,000.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

No comments:

Post a Comment

Pages