Waziri Mkuu Atoa Rai Kwa Waliopata Ufadhili Wa Mafunzo Ya Ufundi


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana waliopata ufadhili wa Serikali kupitia programu maalumu ya kupata mafunzo ya ufundi stadi watumie vizuri fursa hiyo ili wanufaike.

Amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fungu la fedha kwa ajili ya kuwasomesha vijana katika fani mbalimbali za ufundi stadi kwa muda wa miezi sita.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumapili, Agosti 1, 2021) wakati wa uzinduzi wa chuo cha Ufundi Stadi kilichopo katika kijiji cha Kipapa kata ya Lufilyo wilaya ya Busokelo mkoani Mbeya.

“Kilichotuleta hapa ni kuja kushuhudia vijana wetu wa Kitanzania ambao wameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuwapatia ujuzi ili wakaendeleze kazi hizo.”

Amesema Tanzania nzima kuna vijana takribani 45,000 ambao wamesambazwa katika vyuo vyote vya Serikali na vya binafsi ambapo watapatiwa mafunzo ya ufundi stadi kwa miezi sita.
 
Waziri Mkuu amesema mbali na kupatiwa ujunzi katika vyuo hivyo pia vijana wengine wamepelekwa kwenye maeneo ya kutolea huduma kama za utalii, hoteli ili wapate ujuzi.

Amesema chuo hicho cha VETA Busokelo ni kimojawapo kati ya vyuo walivyovichagua ili kipokee vijana wa maeneo ya wilaya za Rungwe, Kyela, Chunya na Mbeya ili kuwapa ujuzi.

“Matarajio yangu vijana wote waliopata nafasi hii hawataipoteza, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anatamani kuona kila Mtanzania akijishughulisha na shughuli za ujasiriamali.

Amesema mkakati wa Serikali kwa mwaka 2021 ni kusomesha vijana 80,000 ambapo asilimia 60 ya mafunzo hayo watayapata kwa vitendo na asilimia 40 watafundishwa darasani.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema chuo cha Ufundi Stadi cha Busokelo kimedahili wanafunzi 127 ambao watapa mafunzo ya ufundi kupitia program hiyo.

Alisema kati ya wanafunzi hao 26 wanasomea ufundi seremala, 45 ushonaji nguo, 28 umeme wa majumbani, 18 ukarabati wa vitarakimishi na 10 utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki.

Alisema mafanikio ya programu hiyo ni pamoja na kuwawezesha wanafunzi waliopata ujuzi kuweza kujiajiri katika fani za useremala, ushonaji, udereva na matumizi ya vitarakinishi.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments