RAIS SAMIA APONGEZA JITIHADA ZA BENKI YA CRDB KUCHANGIA MAENDELEO KATIKA JAMII


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (katikati) akikata utepe kuzindua Afisi ya Maendeleo kata ya Kizimkazi Dimbani na nyumba mbili za madaktari zilizonjengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB na kugharimu shilingi milioni 300. Wengine pichani ni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Haroun Ali Suleiman (watatu kulia), Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid (wakwanza kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Hussein Laay (wapili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wapili kulia) na Mwenyekiti wa CRDB Bank Foundation, Martin Warioba (wa kwanza kulia).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (watatu kulia) akikata utepe kuzindua Afisi ya Maendeleo kata ya Kizimkazi Dimbani na nyumba mbili za madaktari zilizonjengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB na kugharimu shilingi milioni 300. Wengine pichani ni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Haroun Ali Suleiman (wapili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid (wakwanza kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Hussein Laay (watatu kushoto), Mwenyekiti wa CRDB Bank Foundation, Martin Warioba (watatu kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wanne kushoto).
Zanzibar, 28 Agosti 2021 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amepongeza jitihada zinazofanywa na Benki ya CRDB katika kuchangia maendeleo katika jamii. Rais Samia ametoa pongezi hizo wakati wa kilele cha Tamasha la Kizimkazi alipokuwa akikabidhiwa miradi ya nyumba za madaktari na ofisi za shehia Kizimkazi Dimbani zilizojengwa kwa udhamini wa Benki hiyo.

Akipokea miradi hiyo iliyo gharimu kiasi cha shilingi milioni 300, Rais Samia alisema Serikali inajivunia ushirikiano wa kimaendeleo baina yake na Benki ya CRDB. Aliongezea kuwa Benki hiyo imekuwa mfano mzuri wa ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma (PPP) katika kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Maendeleo ya 2025.
“Suala la kuijenga nchi yetu ni wajibu wa kila mmoja wetu na si la Serikali peke yake, niwapongeze Benki ya CRDB kwa kujitoa kwenu kutatua changamoto zilizopo katika jamii. Leo hii mmetutoa kimasomaso kwa kutusaidia kuimarisha sekta ya afya na kuhakikisha wananchi wa Kizimkazi Dimbani wanapata huduma bora za kijamii, ama hakika hii ni Benki ya kizalendo,” alisema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alisifu mafanikio ya Tamasha la Kizimkazi kwa mwaka huu 2021 ambalo lililenga katika kuhamasisha jamii kudumisha utamaduni na kuongeza ujumuishaji wa kiuchumi kwa wananchi kwa kuonyesha fursa mbalimbali zitokanazo na tamaduni za Kitanzania. Tamasha hilo lilihusisha mafunzo kwa wajasiriamali zaidi ya 500 juu ya ubunifu wa bidhaa za asili, elimu ya fedha na uendeshaji biashara, pamoja na michezo mbalimbali ya asili.
Pia alieleza kwamba wakati umewadia kwa Watanzania kuacha utamaduni wa kigeni na kujivunia utamaduni wetu. Alitoa rai kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa na mikakati mbalimbali itakayosaidia kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuenzi na kulinda utamaduni wa Kitanzania. Rais Samia alisema jamii pia ina wajibu wa kushiriki kikamilifu katika matamasha ya utamaduni ili kusaidia ukuzaji na uendelezaji wa mfumo wa utamaduni na sanaa katika jamii ya Kitanzania.

“Benki ya CRDB imetuonyesha kwa mfano kuwa tukiwekeza katika utamaduni wetu tutafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa kutengeneza soko kwa bidhaa zetu za asili na Sanaa yetu. Kupitia Tamasha hili la Kizimkazi niiombe Wizara iweke mikakati ya kuanzisha matamasha ya utamaduni katika kila kanda hii itasaidia kukuza tamaduni za maeneo mbalimbali na kuchochea utalii,” alisisitiza Rais Samia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulamjaid Nsekela alisema utekelezaji wa miradi hiyo na uandaaji wa Tamasha hilo la Kizimkazi ambalo zamani lilikuwa likijulikana kama “Kizimkazi Day,” ni muendelezo wa utekelezaji wa Sera ya Benki hiyo ya uwekezaji katika jamii ambayo inaelekeza asilimia 1 ya faida ya Benki kila mwaka kwa ajili ya kusaidia jamii kupitia program bunifu za uwezeshaji.

Nsekela alisema Benki hiyo imedhamiria kwa dhati kusaidiana na Serikali kujenga uchumi jumuishi na kuwa utamaduni ni moja ya eneo ambalo Taifa likiwekeza vizuri linaweza kusaidia kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Pato la Taifa kwa ujumla. “Pamoja na vijielezi vingi vya neno utamaduni, sisi Kama Benki ya kizalendo tunaamini kuwa; utamaduni ni ujasiriamali, utamaduni ni utalii, utamaduni ni ajira, utamaduni ni uchumi.”

Aidha Nsekela alibainisha kuwa Benki hiyo imedhamiria kuweka mchango wake katika pande zote za Muungano na hivyo kuchochea maendeleo ya Taifa. Akielezea mchango wa Benki hiyo katika kukuza uchumi wa visiwa vya Zanzibar, Nsekela alisema katika nusu mwaka 2021 pekee Benki ya CRDB imetoa zaidi ya shilingi bilioni 150 kuwezesha sekta mbalimbali za maendeleo ili kuwezesha ajenda ya Serikali ya kujenga Uchumi wa Buluu.

Alimwambia Mheshimiwa Rais, Benki hiyo pia inajivunia zaidi kuleta mapinduzi makubwa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mwaka 2014 Benki ya CRDB iliunganisha mfumo wake wa kielekroniki wa ukusanyaji mapato na mfumo wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, ambapo ndani ya mwaka mmoja tu makusanyo yaliongezeka kwa zaidi 600%,” aliongezea.
Nsekela alimuahidi Mheshimiwa Rais kuwa Benki ya CRDB kupitia kauli mbiu yake ya “Tupo Tayari” itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa maendelo nchini ili kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.

Pamoja na mafunzo ya ujasiriamali yaliyoendeshwa na Benki ya CRDB, Tamasha la Kizimkazi pia lilijumuisha usafi wa mazingira, mashindano ya michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu na pete, kufua na kukuna nazi, nage, karata , bao, kuvuta kamba, resi za baskeli, resi za ngalawa, shomooo , na mashindano ya kuhifadhi Qurani.

Wananchi pia walipata fursa ya kupata chanjo ya UVIKO 19 ambayo itatolewa katika viwaja vya Kizimkazi Dimbani Mji Mpya, zoezi ambalo liliongozwa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mh. Ahmed Nassor Mazrui.

Kilele cha Tamasha la Kizimkazi kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakiwa kwenye sherehe hizo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments