MTAMBO WA KISASA WA KUKAUSHA NGUZO ZA UMEME WAZINDULIWA MUFINDI

 Mtambo wa kwanza wa kisasa wa kukausha nguzo katika nchi za Afrika Mashariki na Kati umezinduliwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani wilayani Mufindi Mkoa wa Iringa.

Hafla ya kuzindua mtambo huo ilifanyika katika kiwanda cha nguzo cha Sao Hill kilichopo wilayani Mufindi tarehe 29 Agosti, 2021 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Iringa wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Saad Mtambuli na Mbunge wa Mafinga, Cosato Chumi.

Akitoa taarifa kuhusu mtambo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Sao Hill, Godlisten Minja alisema kuwa maamuzi ya kufunga mtambo kwenye kiwanda hicho yamefanyika ili kuongeza ubora wa nguzo na kuongeza uzalishaji.

Alisema kuwa kwa kutumia mtambo huo nguzo zinakaushwa kati ya siku nne hadi 12 kutegemea hali ya ubichi tofauti na kutumia jua kukausha nguzo hizo ambapo nguzo hukaushwa kwa takriban miezi mitatu hadi minne.

Aliongeza kuwa mtambo huo una uwezo wa kukausha nguzo 800 hadi 900 kwa wakati mmoja kutegemeana na ukubwa wa nguzo.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani aliipongeza Sao Hill kwa kufunga mtambo huo wa kisasa ambao haukuwepo hapa nchini na kufanya upanuzi wa uzalishaji wa nguzo katika kiwanda hicho.

Aliwahakikishia wazalishaji hao na wengine uhakika wa soko la nguzo hizo kwani kazi ya usambazaji umeme mijini na vijijini inaendelea. Aliwataka pia kuongeza uzalishaji wa nguzo hizo.

Alisema kuwa Serikali inategemea kuwa bei ya nguzo hizo zitapungua kutokana na kuongezeka kwa viwanda vya nguzo ambavyo kwa sasa ni zaidi ya 11 .

Aidha alisisitiza kuhusu ubora wa nguzo zinazozalishwa nchini na uhakika wa upatikanaji wa nguzo hizo ili kutokwamisha kazi ya usambazaji umeme.

Aidha, alisisitiza Shirika la Umeme Tanzania na Wakala wa Nishati Vijijini kuhakikisha kuwa nguzo zinazotumika kwenye miradi ya umeme zinakuwa na ubora stahiki na wahakikishe malipo ya nguzo yanafanyika kwa wakati.

Vilevile alisema kuwa mahitaji ya nguzo kwa mwaka ni takriban milioni 4.5 wakat uzalishaji ni milioni 13 hivyo hakuna visingizio vya kutokuwepo kwa nguzo nchini.

Awali, Waziri wa Nishati pia alizindua kiwanda cha kutengeneza nguzo cha Qwihaya kilichopo katika Kijiji cha Mtwango, Wilaya ya Njombe mkoani Njombe.

Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha nguzo 1500 kwa siku na hadi sasa kiwanda hicho kina idadi ya nguzo 400,000.

Uwepo wa kiwanda hicho umeleta manufaa kwa wakulima wa miti ya nguzo katika mikoa ya Ruvuma na Njombe kwani wanauza mazao yao kwenye kiwanda hicho.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post