ATUPWA JELA MAISHA BAADA YA KUMBAKA MTOTO WA MWAKA MMOJA NA MIEZI 7

 Na Amiri Kilagalila,Njombe
 Mahakama ya wilaya ya Njombe imemuhukumu kifungo cha maisha jela Steward Mkongwa (33) kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi saba.

 Katika shauri namba 42 la mwaka  2021 mshtakiwa anadaiwa kufanya kosa la ubakaji kinyume na kifungu cha sheria namba 130 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili lakini pia kifungu 131 kifungu kidogo (1)(3) vya kanuni ya adhabu sura namba 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

 Inadaiwa kuwa mnamo tarehe  26 mwezi Julai mwaka 2020 katika mtaa wa Mwembetogwa halmashauri ya wilaya ya Makambako wilayani Njombe mshtakiwa alimbaka mtoto mwenye umri huo.

 Shauri hilo lililosimamiwa na wakili wa serikali Matiko Nyangero lilikuwa na mashahidi wanne upande wa mashtaka na shahidi mmoja upande wa utetezi ambaye ni mshtakiwa katika kesi iliyoendeshwa na hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Njombe Isaack Mlowe.

 Haimu Mlowe alisema mshtakiwa alikiri kufanya kitendo hicho cha kumuingilia mtoto huyo baada ya mama yake kwenda kuchota maji.

 "Alifanya hivyo kwasababu yeye alikuwa mpangaji pamoja na mama wa huyo pia alikuwa na mazoea na huyo mtoto" alisema Mlowe.

 Kabla ya hukumu hiyo mshtakiwa alipopew nafasi ya kujitetea alisema yeye ana familia inamtegemea kwani ana watoto wawili wa kuwazaa na watoto sita aliyeachiwa na marehemu kaka yake.

 Alisema mke wake aliachana nae kutokana na mitafaruku mbalimbali hivyo mpaka sasa hafahamu watoto hao wanakula ama la.

 "Mimi mwenyewe miguu yangu yote miwili ni mibovu kutokana na kuwa nilipata ajali" alisema Steward.

 Baada ya utetezi huo hakimu Mlowe alimuhukumu mshtakiwa huyo kifungo cha maisha kutokana na kifungu cha sheria namba 131(3) kinachosema mtu yeyote anapotiwa hatiani kwa kosa la ubakaji kwa mtu mwenye umri wa miaka chini ya kumi adhabu yake ni kifungo cha maisha.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments