SERIKALI YAAGIZA ASKOFU GWAJIMA AKAMATWE


Kushoto ni Waziri wa Afya Dkt.Dorothy Gwajima, na kulia ni Mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima
 ***
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, ameliagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kumtafuta na kumkamata popote alipo mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima ili athibitishe kauli anazozitoa dhidi ya Serikali na viongozi kuhusu chanjo ya Covid-19.

Waziri Gwajima ametoa agizo hilo leo Jumanne, Agosti 17, 2021 akiwa katika kijiji cha Kyatunge Wilaya ya Butiama mkoani Mara na kueleza kuwa Askofu Gwajima amekuwa akitoa taarifa za upotoshaji kwa makusudi kuhusu chanjo ya Corona jambo ambalo linaivuruga wizara yake na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari duniani.

Maagizo hayo ya Waziri Gwajima yanakuja ikiwa ni saa chache tangu Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel kumtaka Askofu Gwajima kujitafakari juu ya madhara yatakayowakuta wananchi kutokana na upotoshaji anaoendelea kuufanya na kuongeza kuwa hawezi kupingana na Serikali na hana uthibitisho wa kisayansi kuhusu chanjo ya corona.

“Gwajima amevuka mipaka, anapotosha Taifa, hawezi kupingana na serikali na hana uthibitisho wa kisayansi, anasema mtu akichanjwa kuna vitu vinaingizwa mwilini ili mtu afe baada ya miaka miwili ama kumi, tutamuita athibitishe hili, akishindwa tutamshughulikia.

“Nimekuja kumuonya nikiwa kama mwana sayansi, ili ajue kwamba ametukanyaga sehemu, Gwajima anajua ukweli lakini ameamua kucheza ligi, tunamuonya tunataka awe na uthibitisho wa Kisayansi kwa kile anachosema kuhusu Chanjo ya Corona.

“Tumetumia nguvu nyingi sana kumuelimisha (Askofu Gwajima), tunataka tuthibitishiane kwamba sisi na yeye nani anataka kuiangamiza nchi, tujue nani anataka kuilinda nchi,” alisema Dk. Mollel.

Askofu Gwajima na waumini wake amejipambanua kukataa chanjo ya corona iliyoletwa nchini kwa madai kuwa haijathibitishwa mamlaka husika za afya huku akiongeza kuwa zina madhara na zinaweza kuwaletea matatizo makubwa wananchi wa Tanzania huku akiitaka Serikali kujiridhisha na usalama wa chanjo hizo.

“Mimi namtaka daktari atakayeshadadia nitakula naye meza moja. Utakufa daktari, utaona,” alisema Askofu Gwajima huku akishangiliwa na waumini wake.

Aliendelea: “Daktari yoyote wa Kitanzania atakayeanza kushadadia watu wachanjwe na yeye mwenyewe hajafanya utafiti wa kuna nini ndani ya chanjo, madhara ya muda mfupi, madhara ya muda mrefu kwetu na watoto wetu na nchi yetu. Nasema hivi kufa na ufe kwa jina la Yesu.”

Aidha, Askofu Gwajima alidai kwamba janga la virusi vya corona lina uhusiano na juhudi za kusambaza teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ya 5G huku akiongeza pia kuwa watakaochanjwa huenda vizazi vyao vikabadilika miaka kadhaa ijayo na kuwa mazombi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post