IJUE ASILI YA JINA MAARUFU 'GAMBOSHI' ...MTI WA MATAMBIKO


Mti aina ya Ninje katika kaburi la Gamboshi ambaye ni mwanzilishi wa kijiji cha Gamboshi kilichopo wilayani Bariadi mkoani Simiyu, Sehemu hiyo hutumika pia kwa ajili ya matambiko ya mila na desturi katika kabila la wasukuma hasa kuomba Mvua kipindi cha masika inapokosekana. (Picha zote na  Costantine Mathias)


Na Costantine Mathias - Gamboshi
Umaarufu wa kijiji cha Gamboshi ni mkubwa kuliko hata umaarufu wa viongozi waliopigania Uhuru barani Afrika, Umaarufu huu unatokana na kijiji hicho kujulikana kwa masuala ya ushirikina.

Wengi ambao hupata simulizi ama za kweli au za kutunga, huamini kuwa kijiji hicho ni cha washirikina na hakina maendeleo kutokana na ukweli kwamba hawajawahi kufika huko.

Lakini hali iliyoko katika kijiji hicho kwa sasa ni tofauti na mtizamo wa jamii iliyoko nje, shughuli za kilimo, biashara, ufugaji pamoja na huduma za kijamii zinafanyika katika jamii hiyo.

Wananchi wa kijiji hicho ni wacheshi, wachapa kazi na wanajali wageni kwa kuwapa historia ya kijiji hicho huku wakitumia nafasi hiyo kuwaondolea dhana iliyojengeka kuwa ni kijiji cha wachawi.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, kijiji cha Gamboshi kilikuwa na jumla ya watu 4,232, kaya 618 na vitongoji vinane na utoaji wa huduma za kiroho (makanisa) umeshamiri kijijini hapo.

Ukiwa mgeni katika eneo hilo lazime uwe na hofu ya kutembelea kijiji hicho, kwani hutakuwa na imani kama utakwenda na kurudi salama kutokana na imani zilizojengeka ilhali wanaofika huko hurudi salama.

Mwandishi wa habari hizi alifunga safari kuelekea kijijini hapo mwendo wa masaa mawili kutoka Bariadi mjini, ili kuweza kupata historia na masimulizi ya kijiji hicho kwa lengo la kuhusianisha na uvumi ulioko nje ya maeneo hayo.

Kutoka Bariadi mjini unapita kijiji cha Ngulyati kiasi cha kilometa 30 Mashariki ya Bariadi katika barabara itokayo Bariadi kwenda Magu, lakini hakuna kibao kinachotambulisha Kijiji cha Gamboshi mwanzoni mwa barabara ya vumbi inayoelekea Gamboshi kutoka Ngulyati.

Upande wa kaskazini kijiji hicho kinapakana na kijiji cha Kisesa kilichopo wilaya ya Busega, kusini kinapakana na Nyamswa, Magharibi kijiji cha Lulayu, kusini- Magharibi kijiji cha Ditima na Mashariki kijiji cha Miswaki.

Asili ya jina Gamboshi.

Wenyeji wa kijiji hicho wanasimulia kuwa jina Gamboshi ni sawa na majina ya vijiji au miji mingine na kwamba jina hilo halihusiani na masuala ya ushirikia wala uchawi.

Mabula Bahati Magamula mkazi wa kijiji hicho anasema jina Gamboshi ni sawa na majina ya vijiji vingine, jina ambalo lilitokana na muwindaji wa wanyama pori aliyekuwa anauwa wanyama na alitambulika kwa jina la Masuku Ga mbushi 'Gamboshi'.

Inaelezwa kuwa Masuku Ga Mbushi yule muwindaji alipokufa watu walikula nyama nyingi za nyumbu (mbushi), jamii  ya Wanyantuzu ilibaki na kumbukumbu kwa miaka ikafikia kusema Gambushi  /Gamboshi/Gambosi

"Gamboshi"...Kila eneo wanaita jina kutokana na tukio, katika kijiji chetu mtu wa kwanza alijulikana kwa jila la Gamboshi alitokana na umaarufu wa uwindaji, wananchi walikuwa wanakuja kununua nyama pori (manda) kwa Gamboshi’’ anasema Magamula.

Magamula anasema jina hilo lilipata umaarufu miaka ya 1960’s ambapo Gamboshi alikuwa mwenyeji wa mkoa wa Mara (Mshashi), hivyo kutokana na umaarufu wake na watu kuwauzia nyamapori alifahamika sana.

Anasema jina Gamboshi ni jina kama yalivyo majina mengine na kwamba baada ya kufariki alizikwa kijijini humo na watu wa eneo hilo hufanya matambiko katika kaburi lake kwa ajili ya kuomba mvua.

"Mvua ikigoma huwa tunafanya matambiko katika kaburi la Gamboshi ambaye ni mwanzilishi wa kijiji hiki, kutokana na imani tuliyonayo tunapata mvua…Imani huponya ukitoa wanaoamini katika Ukristo, wanaobaki hufanya matambiko’", anasema Magamula.

Magamula anaendelea kufafanua kuwa mila na desturi za mbina ziliweza kueneza masimulizi juu ya uchawi wa kijiji cha Gamboshi kutokana na mchezo huo uliokuwa unabeba viashiria vya uchawi.

Anasema katika miaka ya 1960 mpaka 70 walikuwepo wakina mama wawili (Mwana Mabula na Mwana Makulyu) ambao walikuwa wanafanya michezo ya asili iliyojulikana kama mbina ambayo waliicheza kwa kutumia dawa za asili.

Anasema mbina za kila mwaka zilichezwa katika kijiji hicho na miujiza mingi ilikuwa ikitolewa siku ya mbina ambapo kila upande ulishindana kuvutia watazamaji.

"Mbina za Wagika na Wagalu zilikuwa itikadi, mila na desturi za enzi na enzi za mababu wa jamii ya kabila la wasukuma..kwa sababu mbina ilikuwa haiwezi kuchezwa na watu wa eneo moja, hivyo wakina mama hao walialika pia watu kuwasaidia", anasema.

Anaeleza kuwa hata kama wachezaji wengine watatoka vijiji jirani, wakija na miujiza (mabinda) yalifahamika kuwa ni ya haohao akina mama, hali iliyoifanya Gamboshi kujulikana kwa uchawi na miujiza.

Anatolea mfano, ‘’siku ya mbina upande mmoja inaweza kunyesha mvua wakati sehemu nyingine jua linawaka, upande mwingine wanaweza kutokea siafu au vyura hali inayowafanya watazamaji kushangaa na kuvutiwa na miujiza hiyo…watazamaji waliendelea kusimuliana maajabu ya Gamboshi na kueneza kuwa ni kijiji cha wachawi’’

Magamula anasema kutokana na ushirikina wa akina mama hao pamoja na kuonyesha michezo ya kushindania dawa, walijulikana sana kila kona kwa maajabu ya siku za mbina na simulizi kuliko uhalisia.

Anasema Mamanju wa mbina pia walichangia kueneza masimulizi ya ushirikina kutokana na nyimbo walizokuwa wanatunga hali iliyoamusha ari na kukifanya kijiji chao kutengwa sababu ya simulizi hizo.

Seni Lyochi anasema familia yao ilihamia katika kijiji cha Gamboshi miaka ya 1975 na kukuta umaarufu wa Gamboshi, jina la mtu lililotumika kubeba jina la kijiji kizima.

"Mwanzilishi wa kijiji hiki aliitwa Gamboshi, alikuwa muwindaji wa wanyamapori, watu walisimuliana…Tunaenda kwa Gamboshi kununua nyamapori, alifahamika sana sababu ya nyamapori", anasema Lyochi.

Anaeleza kuwa matambiko yana sababu zake na hufanyika kulingana na imani, mila na desturi za eneo husika ili kuomba mahitaji yenu na hutokea kuomba au kufanya matambiko pindi mnapokuwa na tatizo la ujumla.

Wilson Heka anasema uwepo wa huduma za kiroho umetokomeza imani potofu na kwamba maisha ya wakati huo na sasa yamebadilika sana kutokana na eneo hilo kupatiwa huduma za kijamii.

Anasema elimu imeondoa mitizamo hasi ya kishirikina katika kijiji hicho na maeneo jirani na kwamba miaka ya nyuma kila ukitaja Gamboshi watu wanakutafsiri tofauti.

Ninje, Mti wa Imani Gamboshi.
Wenyeji wa Gamboshi wanasema baada ya Gamboshi kufariki alizikwa Kaskazini mwa kijiji hicho na katika kaburi lake uliota mti mkubwa unaoitwa Ninje, ambao hutumika kuabudia.

Wanasema matunda, majani, magome na mizizi ya mti huo hutumika kwa ajili ya tiba ya magonjwa mbalimbali ikiwemo tumbo, pia matunda na mti huo hutumika kuongeza maziwa kwa akina mama wanyonyeshao.

Pia matunda ya mti huo hutumika kuongeza uzalishaji wa mazao shambani hasa katika mashamba ya viazi kiasi kwamba viazi huiva kwa kama lilivyo tunda la mti wa Ninje.

Lyochi anasema matambiko yana muda, sehemu na sababu zake kulingana na imani na desturi za kila jamii na kwamba kabla ya ujio wa dini watu wengi walikuwa wakifanikiwa kupitia mitambiko.

"Tunaenda kwa mwazilishi (Ntale) kwa ajili ya kuomba neema, baraka pamoja na mvua…hata sisi wana Gamboshi tunaenda alipozikwa mwanzilishi wetu kwa ajili ya kuomba mvua", anasema Lyochi.

Magamula anasema mti huo hutumika kuomba na kufanya matambiko ya kimila hasa majira ya mvua pindi ikigoma kunyesha, na kwamba wazee wa mila na desturi kukutana na kufanya mitambiko hiyo.

Hata hivyo Mwandishi wa habari hizi alifanikiwa kufika katika eneo alilozikwa Gamboshi na kukuta mti wa Ninje ukiwa katikati ya shamba la viazi na kwamba eneo hilo halitumiki kwa shughuli zozote bali limehifadhiwa kwa matumizi maalum.

Eneo hilo linaonekana hutumika kwa ajili ya matambiko ya kimila sababu limezungushiwa katani za asili (mkonge) pamoja na mawe huku katikati kukiwa na mti wa Ninje.

Soma pia:

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments