WAVUTA SIGARA/TUMBAKU WABANWA


Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetoa muda wa mwaka mmoja kuanzia Julai 26, 2021 kwa wamiliki, wapangaji na waendeshaji wote wa maeneo panaporuhusiwa kuvuta sigara (taasisi za elimu ya juu, majengo ya ofisi, hoteli, baa, migahawa na maeneo ya burudani) kutenganisha vyumba au maeneo maalum ya kuvutia na kutovutia sigara.

Aidha, TMDA imesema kuwa Kanuni za Bidhaa za Tumbaku za mwaka 2014 inawataka wamiliki wote wa majengo yanayotumiwa na watu wengi kuweka vifaa vya kubaini moshi wa tumbaku na kuweka alama zinazosomeka ‘Jengo Hili Limefungwa Mitambo ya Kubaini Moshi wa Tumbaku.’

Mamlaka hiyo imefafanua kuwa baada ya muda huo, ukaguzi utafanyika nchi nzima ili kuhakiki utekelezaji wa maelekezo hayo ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa wale ambao hawatotii.

Pia, imekumbusha kuwa Sheria ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku inazuia uvutaji wa tumbaku katika maeneo ya umma ambayo ni pamoja na sehemu zinapotolewa huduma za afya, maktaba, sehemu za ibada au mikutano au shughuli za michezo na burudani na sehemu za maduka makubwa. Katika maeneo hayo sheria inataka kuwekwa bango litakalosomeka ‘Hauruhusiwi Kuvuta Sigara.’

TMDA imetahadharisha kuwa maelekezo hayo yanahusu bidhaa za tumbaku zinazotambulika kisheria ambazo ni sigara, siga, sigarusi, misokoto, shisha, kiko na tumbaku ya unga pekee.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments