WANANCHI WATAKIWA KUPATA RAMANI ZINAZOTOLEWA NA WIZARA YA ARDHI

Na Munir Shemweta
Wakati Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara yakiendelea katika viwanja vya Mwl. Nyerere Dar es Salaam wananchi wametakiwa kutembelea Banda la Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kujipatia Ramani za Tanzania na ile ya jiji la Dar es Salaam.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia idara yake ya Upimaji na Ramani ndiyo yenye jukumu la kutoa Ramani ya Tanzania, mikoa pamoja na zile za wilaya kwa kuwa ndiyo yenye mamlaka ya kupima mipaka yote ikiwemo ya nchi kavu na majini.

Akizungumza katika maonesho ya Sabasaba tarehe 1 Julai 2021 mkoani Dar es Salaam Afisa Upimaji wa Wizara ya Ardhi Vicky Sonda alisema, wananchi wanaotembelea Banda la Wizara mbali na huduma nyingine wataweza kujipatia Ramani za Tanzania pamoja na zile za jiji la Dar es Salaam.

Alisema, Ramani za jiji la Dar es Salaam zinazopatikana kwenye Banda la Wizara katika Maonesho ya Sabasaba zitawasaidia wananchi hasa wageni kujua maeneo mbalimbali ya jiji kwa haraka bila kulazimika kuuliza.

"Ramani za jiji la Dar es Salaam zinazopatikana hapa zitaweza kumsaidia mwananchi kutambua eneo analoenda kwa uharaka bila kuuliza" alisema Vicky

Kwa mujibu wa Vicky, wananchi watakaotembelea Banda la Wizara pia watajua uhalali wa umiliki wa tanzania maeneo ya mipaka ya bahari kupitia ramani alizozieleza kuwa zinaonesha maeneo ya mipaka baina ya Tanzania na nchi nyingine.

Aidha, Afisa huyo Upimaji kutoka Wizara ya Ardhi Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam alisema kuwa, fursa nyingine wanayoweza kunufaika wananchi wanaotembelea banda la wizara ya Ardhi ni kufahamu uwepo wa kisiwa ndani ya kisiwa cha Mafia  kinachoitwa Bwejuu.

"Wananchi watakaotembelea Banda letu watapata fursa ya kufahamu uwepo kisiwa ndani ya kisiwa cha Mafia kinachoitwa Bwejuu na kisiwa hicho ni maarufu sana kwa shughuli za utalii" alisema Vicky.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea kutoa huduma mbalimbali katika maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara ikiwemo kutoa hati za papo hapo kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments