NAIBU WAZIRI MABULA APIGA MARUFUKU WANAOSHITAKIANA MABARAZA YA ARDHI KUGHARAMIA USAFIRI


Na Munir Shemweta, SONGWE
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amepiga marufuku wananchi wanaoshitakiana kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya kugharamia usafiri wa kwenda uwandani wakati wa kusikiliza mashauri ya ardhi.

Akizungumza wakati wa kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya, mkoa wa Songwe jana  Dkt Mabula alisema, asingependa kuona wananchi  wanaoshitakiana katika kesi ya ardhi mmoja wao atoe fadhila ya usafiri wa kwenda uwandani.

‘Tusingependa wale wanaoshitakiana mmoja wao atoe fadhila ya usafiri maana baada ya hapo mara nyingi wazee wa Baraza wanashawishika na kuona anayetoa usafiri kuwa amekuwa ni msamamaria mwema kwa hiyo wanamlipa fadhila hata kama hana haki ya kupata ushindi’ alisema Naibu Waziri Mabula.

Aliwataka Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi kuandaa ratiba za mashauri ya Ardhi kwenye maeneo yao na kuzipeleka kwa wakuu wa wilaya aliowaeleza kuwa watashirikiana na wakurugenzi wa halmashauri kuangalia ratiba na kutoa usafiri kwa wazee wa mabarza   ili kwenda uwandani wakati wa mashauri.

Naye Kamishna wa Ardhi Nchini Methew Nhonge alisema pamoja na kuwa sheria ya ardhi imeanisha utaratibu mzuri wa kisheria katika kushughulikia migogoro ya ardhi lakini halmashauri na ofisi za ardhi za mikoa zinao wajibu mkubwa wa kuhakikisha migogoro ya ardhi kabla haijaenda mahakamani inatatuliwa kwa njia ya kiutawala.

‘Bahati nzuri katika wizara tumeweka utaratibu kwa nchi nzima kuhakikisha kwamba viongozi wa ardhi wa mkoa pamoja na halmashauri kupitia watendaji wa sekta wanaenda kwenye ngazi za halmashauri na mitaa kutoa elimu na kushughulikia migogoro ya wananchi kiutawala’’ alisema Nhonge.

 Kwa upande wake Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya nchini Stela Tullo aliushurukuru uongozi wa mkoa wa Songwe kwa kusaidia kupata jengo la Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya na kueleza kwamba, uanzishwaji baraza hilo utasaidia kuondoa usumbufu waliokuwa wakiupata wananchi wa Songwe kusafiri  umbali mrefu kufuata huduma za Baraza mkoani  Mbeya.

‘Ninawasihi wananchi wa Songwe kulitumia vizuri baraza la ardhi la mkoa wa Songwe kupata huduma, ile migogoro ya ardhi iliyoshindwa kusuluhishana nyumbani hata katika ngazi ya familia na mabaraza ya ardhi ya vijiji na kata basi serikali imewasogezea huduma kwenye baraza la ardhi na nyumba la wilaya  mkoa wa Songwe’’ alisema Stela Tullo.

Kabla ya uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, mkoa wa Songwe, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alizindua Baraza kama hilo  wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ambapo aliagiza mashauri ya ardhi yasikilizwe na kuisha katika kipindi kisichozidi miaka miwili.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments