KAULI YA SERIKALI KUHUSU SAMAKI WALIOKUTWA WAMEKUFA UFUKWENI DAR ES SALAAM


Tarehe 21 mwezi Julai, 2021 saa 3:30 asubuhi, ofisi ndogo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mkoa wa Dar es Salaam ilipokea taarifa kutoka kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala kuhusu tukio la kuelea kwa samaki waliokufa katika ufukwe uliyopo karibu na Hospitali za Agha Khan na Ocean Road jijini Dar es Salaam.


Kufuatia taarifa hiyo maafisa uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliuomba uongozi wa kipolisi Ilala kuimarisha ulinzi eneo hilo ili kuzuia wananchi kuchukua samaki waliokuwa wakielea ufukweni hapo wakati hatua zaidi za haraka zikichukuliwa kuzuia uingizaji wa samaki hao katika Soko la Magogoni Feri lililopo karibu na eneo la tukio.


Baada ya kuimarisha ulinzi eneo la Soko la Magogoni Feri na eneo la tukio, wananchi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, maafisa wa wizara, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), maafisa uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wakiwa na meneja wa Soko la Magogoni Feri walikusanya samaki kiasi cha Kilogramu 164 na kufikisha Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Baada ya kutolewa kwa ufafanuzi wa hali iliyojitokeza ilikubaliwa kuwa sampuli za samaki hao zichukuliwe kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara ili kubaini sababu za vifo vya samaki hao.


Sampuli zilichukuliwa kwa ajili ya maabara ya TAFIRI, maabara ya Taifa ya Uvuvi (Dar es Salaam) na Polisi Kitengo cha Sayansi ya Uchunguzi (Forensic Investigation) kwa ajili ya kupeleka maabara ya mkemia mkuu wa serikali.


Kiasi cha Kilogramu 156 kilichosalia kilikabidhiwa kwa afisa uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuteketezwa na tukio la kuteketezwa lilishuhudiwa na maafisa wa wizara, uongozi wa Soko la Feri, ofisi ya uvuvi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na wananchi waliokuwepo eneo la Soko la Magogoni Feri.


Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi inapenda kuwashukuru wananchi wote waliokuwepo kwenye ufukwe wa hospitali za Agha Khan na Ocean Road pamoja na Soko la Magogoni Feri wakati wa tukio hili kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha uliofanikisha kuzuia kuingizwa kwa samaki hao sokoni na hatimaye kuteketezwa na afisa uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.


Aidha, Wizara inapenda kuwaasa wananchi kuendelea na biashara ya samaki katika masoko ya Jiji la Dar es Salaam kama ilivyo kawaida na umma utajulishwa kuhusu sababu za vifo vya samaki hao walioteketezwa mara baada ya kupatikana kwa mujibu wa uchunguzi wa kimaabara.


Imetolewa:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments