VIJANA WA CCM SHINYANGA WAMUOMBA RAIS SAMIA KUTAZAMA UPYA SUALA LA TOZO YA MIAMALA YA SIMU...'LINAUMIZA'


Mwenyekiti wa UVCCM, Baraka Shemahonge akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Vijana wa CCM mkoa wa Shinyanga.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Shinyanga likiongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM, Baraka Shemahonge wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kulitazama kwa taswira mpya suala zima la tozo za miamala ya simu kwa manufaa ya wananchi wa hali ya chini na Ajira za vijana wengi wanaojipatia kipato kutokana na shughuli za kutuma miamala kwani mzunguko miamala ya simu za mkononi utapungua.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa UVCCM, Baraka Shemahonge Julai16,2021 katika kikao cha Baraza la Vijana wa CCM mkoa wa Shinyanga ambacho kimehudhuriwa na mkuu wa mkoa huo Dkt. Philemon Sengati aliyekuwa mgeni rasmi katika kikao hicho pamoja na Naibu Waziri wa Vijana Kazi na Ajira, Patrobas Katambi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini na Mbunge wa Kundi la Vijana Mwasi Kamani.

“Baraza la Vijana linampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya tangu kuingia kwake madarakani ikiwemo kukuza maendeleo pamoja na kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati nchini .Tangu kuingia kwake madarakani upo mwanga na matumaini kwa wananchi. Tunamuomba Mhe. Rais kulitazama kwa taswira mpya suala zima la tozo za miamala ya simu”,amesema Shemahonge.

Shemahonge amesema wanamuomba Mhe. Rais Samia alitazame upya jambo la Tozo za miamala ya Simu akibainisha kuwa wana imani kila Mtanzania yuko tayari kuchangia maendeleo ya nchi yake kwani Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe lakini tozo imekuwa kubwa kidogo.

“Tunaona vijana wengi watakosa ajira kwa sababu mzunguko wa miamala ya simu utapungua lakini wazee na wananchi waliopo vijijini wataathirika kwa sababu kule hakuna Benki, wengi wao wanatumia Simu kutuma na kutumiwa fedha. Kwa makato haya yanakwenda kuathiri moja kwa moja wananchi wenye kipato chaa chini”,amesema Shemahonge.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemoni Sengati amewaomba vijana wa UVCCM Mkoa kuendelea kuhamasisha Falsafa ya kujitegemea kiuchumi kwa vijana na kuwa wabunifu wa fursa mbalimbali huku akiafiki ombi la ujenzi wa Chuo Kikuu ambacho kitakuwa kichocheo cha uchumi wa mkoa wa Shinyanga.

Dkt. Sengati pia amechangia Shilingi milioni 2.5 kwa ajiri ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Vijana wa CCM mkoa wa Shinyanga.

Kuanzia Alhamisi Julai 15, 2021, watumaji na watoaji fedha kupitia simu za mkononi, walianza kulipa kodi ya uzalendo iliyopandisha gharama za kutuma na kutoa fedha mara 11 ya ilivyokuwa mwanzo, hali iliyoelezwa kuacha maumivu kwa wengi.

Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wamesema tozo mpya ni mzigo mwingine kwa wenye kipato cha chini, hasa vijijini ambako simu za mkononi ni mkombozi wa huduma za fedha kutokana na kutokuwepo kwa huduma za benki.

Wamesema tozo hizo ni kubwa na zinashawishi watu kukwepa miamala ya simu na k kuejielekeza katika huduma za benki wakibainisha kuwa Tozo mpya ni maumivu kwa wananchi wa kipato cha chini ambao ndio watumiaji wakubwa wa miamala ya simu huku wengine wakidai kodi hiyo ni ishara ya kutowafikiria wananchi wa kawaida.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments