AMKIMBIA MMEWE BAADA YA KUMFUMANIA NA CHUPI YA MCHEPUKO


Mwanamke mmoja kutoka Nguuni, eneo la Mwingi nchini Kenya  ameamua kumuacha mumewe baada ya kupata chupi ya mwanamke mwingine kwenye mfuko wa koti lake akifua nguo.

 Inasemekana kuwa jamaa alikuwa amerejea nyumbani siku iliyofuata mapema asubuhi akiwa mlevi chakari.

Kwa mujibu wa Taifa Leo, mrembo alimlaki mumewe na kumkaribisha nyumbani akamvua nguo chafu kisha akamtandikia kitanda alale ili stimu za pombe zimtoke mwilini.

 Inasemekana kwamba mzee alipokuwa akisukuma usingizi mkewe alianza kufua nguo na hapo ndiposa alipata chupi kutoka kwenye mfuko wa koti la mumewe.

Mama alipandwa na mori kutokana na kila alichokiona ambapo alifululiza hadi chumba alichokuwa amelala mumewe na kumwamsha kwa fujo.

“Wewe ulikesha kwa nani na chupi hii ni ya nani? Amka haraka wacha kujifanya hujui ninachokuuliza,” dada huyo alimcheka.

Jamaa aliropokwa kilevi bila kujua njama yake ya kuchepuka na wanawake wengine ilikuwa imefichuka baada ya chupi ya mpango wake wa kando kumsaliti ilipopatikana kwenye koti lake.

Hata hivyo, jamaa alikana chupi ilikuwa ya mpango wake wa kando. “Chupi gani hiyo? Chupi hiyo ni yako si ya mtu mwingine. Wacha kunilaumu bure,” jamaa alisema na kuendelea kulala.

Mwanamke huyo alimgutusha jamaa kwa kumzaba kofi usoni.

 “Amka haraka. Mimi sina chupi ya rangi hii. Wacha kujifanya eti hujui mwenyewe. Tabia yako imenifika kooni na sasa ninaondoka nikuachie mwenye chupi hiyo,” kisura alisema. 

Penyenye zinasema kwamba kipusa huyo alichukua kilichokuwa chake na kuondoka.

Inaarifiwa kwamba kimada wa jamaa aliweka chupi hiyo kwenye mfuko wa koti la jamaa kwa kusudi la kumkosanisha na mkewe.

Chanzo - Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post