Tanzania Na Uturuki Zanuia Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi

 


Na Mwandishi wetu, Dodoma
Serikali ya Uturuki imeahidi kushirikiana na Tanzania kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali zinazoikabili Jamii hapa nchini ikiwemo mapambano dhidi ya ukatili kwa Wanawake na watoto.

Hayo yamebainishwa na Balozi wa Uturuki hapa nchini Dkt. Mehmet Gulluoglu alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu Ofisini kwake Jijini Dodoma.

Dkt.Gulluoglu ambaye pamoja na mambo mengine, amesema nchi yake kupitia wafadhili mbalimbali nchini Uturuki iko tayari kushiriki katika Maendeleo ya Tanzania hususan katika masuala ya Elimu, Uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi na kupambana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia.

 Awali, akizungumzia Shughuli zinazoratibiwa na Wizara yake, Katibu Mkuu Dkt. Jingu alisema Serikali imeanza kuwekeza katika Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi lengo likiwa kuboresha uchumi wa Kaya na hatimaye kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.

" Serikali kupitia Wizara yetu, tumeanza ajenda ya kuwawezesha Wanawake kiuchumi kupitia afua mbalimbali ili kuhakikisha uchumi unapanda kuanzia ngazi ya kaya," alisema Dkt. Jingu.

Amesema katika kuhakikisha mipango hiyo inafakikiwa Serikali kupitia Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wadau mbalimbali imeanza kuwekeza katika Kilimo cha Parachichi kwenye mikoa ya Iringa,Njombe na Mbeya na Kilimo cha Alizeti kwa mikoa ya Singida na Dodoma huku Mkoa wa Kigoma ukitumika kwa Kilimo cha michikichi.

Akizungumzia uboreshaji wa huduma kwa Wazee nchini, Dkt. Jingu amesema suala hilo ni moja ya Vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita ambapo amesema Serikali inahudumia makazi ya Wazee wasiojiweza 13 katika maeneo mbalimbali nchini.

Kuhusu Maendeleo ya Mtoto, amesema Jukumu la Serikali kupita Wizara ni kuhakikisha huduma na haki zao zinapatikana ikiwemo haki kwa watoto waliokinzana na Sheria.

Kuhusu  Mashirika Yasiyo ya Kiserikali,  Dkt. Jingu amesema Wizara inatoa miongozo na kuratibu uendeshaji wake ili kuhakikisha yanafanya kazi kwa misingi ya Uwazi na Uwajibikaji.

Moja ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kimataifa ni Turkish Maarif Foundation  linalijishughulisha na masuala ya elimu ambalo kwa sasa linaendesha Shule katika Mikoa ya Dar Es Salaam, Arusha na Zanzibar.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika hilo, Oguz Hamza amesema lengo lao ni kutoa elimu bora kwa Wanafunzi wa Tanzania kwa gharama nafuu.

Amesema Uturuki kuna Mashirika mengi yanayojihusisha na masuala mbalimbali ya Maendeleo ambayo yanaweza kuratibiwa ili kuongeza huduma zake nchini Tanzania.

Akifafanua kuhusu ushirikiano miongoni mwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Msajili wa Mashirika hayo hapa Nchini, Vickness Mayao amesema suala hilo linahitaji uratibu wa pamoja kulingana na maeneo husika huku vigezo na Masharti yakizingatiwa.

Mayao amesema pia kuwa kuna uwezekano wa Serikali kuingia Makubaliano kuhusu namna ya kushirikiana katika maeneo yanayokusudiwa.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments