UCHAGUZI MKUU WA BARAZA LA TAIFA LA URATIBU WA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI 'NaCoNGO' KUFANYIKA JULAI 8


Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa viongozi (NaCoNGO) Wakili Flaviana Charles ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kutetea Haki za Binadamu na Biashara, (wa pili kulia) akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wao na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam. (kulia kwake) ni Katibu wa Kamati hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga, (wa kwanza kushoto) ni mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la (WISE) Dkt. Astronaut Bagile, na (wa kwanza kulia) ni Mkurugenzi Shirika la (WiLDAF) Wakili Anna Kulaya.
Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa viongozi (NaCoNGO) Wakili Flaviana Charles (kulia) akijadiliana jambo na Katibu wake Francis Kiwanga (kushoto) wakati wa mkutano wao na waandishi wa Habari uliofanyika Juni 16, 2021.
Katibu wa Kamati hiyo Francis Kiwanga (aliyesimama) akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari kwenye Mkutano huo.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa NaCoNGO Wakili Fraviana Charles akizungumza na waandishi wa Habari (hawamo Pichani) kwenye mkutano wao na wanahabari hao jijini Dar es Salaam.
Mjumbe wa Kamati ya uchaguzi wa NaCoNGO Dkt. Astronaut Bagile (kushoto) akizungumza na viongozi wa kamati hiyo, Francis Kiwanga (katikati), na Wakili Flaviana Charles (kulia).

***
Katika kuelekea kufanyika uchaguzi Mkuu wa BARAZA la Taifa la Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), unaotarajiwa kufanyika Julai 8 mwaka huu, Kamati maalum ya kitaifa inayoratibu na kusimamia uchaguzi huo imetoa wito kwa makundi mbalimbali hususani wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Uchaguzi huo Wakili msomi Flaviana Charles, amesema kuwa uchaguzi huo umeitishwa mara baada ya kuundwa kwa kamati hiyo yenye watu 10 kutoka katika mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), ya kitaifa na kimataifa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, ili kusimamia mchakato huo.

Ameongeza kuwa fomu za kuomba kugombea katika nafasi mbalimbali  zitaanza kuchukuliwa rasmi  Juni 21 katika Ofisi zote za Afisa Maendeleo ya Jamii  wa wilaya zote 139 nchini na mwisho wa kurudisha fomu hizo ni Juni 24 mwaka huu.

Aidha Mwenyekiti huyo wa kamati ameongeza kuwa ifikapo Juni 25,kutafanyika zoezi la kuchakata fomu zote za wagombea katika Ofisi hizo na kazi hiyo itafanywa na  kamati hiyo.

"Ifikapo Juni 26,2021uchaguzi katika ngazi za wilaya utaanza huku Juni 28 uchaguzi wa wajumbe wa Baraza katika ngazi ya mkoa ambapo Julai 5 hadi 8,2021 utakuwa ni uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa baraza, kamati ndogo na wajumbe wa bodi ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali,"amesema  

Amesema  kuwa mnamo Julai 9 hadi 10 kutakuwa na uapisho na makabidhiano ya nyaraka na Ofisi na kuanza kazi kwa watumishi hao.

Wakili Flaviana amewalihimiza watu wote wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo kujitokeza kugombea nafasi hizo kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na makundi maalum yakiwemo ya watu wenye ulemavu. 

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Foundation for Civil Society, (FCS) Francis Kiwanga  amesema kuwa  Baraza hilo ni muhimu katika Taasisi hususani katika kazi zote hizo za kusimamia masuala ya uchaguzi.

"Rai yeti sisi kwa Asasi zote za Kiraia kila mtu aweze kushiriki na watu wachukue fomu na kugombea nafasi hizi zilizotangazwa ,"amesema.

"Ushiriki wa wanawake katika uchaguzi huu ni muhimu sana hivyo tunatoa Rai yetu watu wajitokeze ili baraza liwe shirikishi zaidi na wadau wenye upana,"amesema  Kiwanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments