HALMASHAURI YA SHINYANGA YAZINDUA ZOEZI LA UTOAJI WA KINGATIBA YA KICHOCHO NA MINYOO YA TUMBO KWA WANAFUNZI

 

Wanafunzi wa shule ya Msingi Iselamagazi wakipata chakula kwa ajili ya kujiweka sawa ili wapewe kingatiba ya kichocho na  minyoo ya tumbo

 Na Shinyanga Press Club Blog
HALMASHAURI ya Wilaya ya Shinyanga, imezindua zoezi la utoaji wa kingatiba ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ya Kichocho na Minyoo ya tumbo kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Iselamagazi katika halmashauri hiyo.

Uzinduzi huo uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Hoja Mahiba, ambaye amekemea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi wanaowazuia watoto wao kwenda shule ili kukwepa wasipate kingatiba za minyoo ya tumbo na kichocho, huku akiwaondolea wananchi hofu kwani dawa hizo hazina madhara kwa watoto bali zinalenga kuwakinga na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.

Aidha Mahiba ameagiza viongozi wa kata na vijiji kufanya ufuatiliaji na kuwachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya watu wanaoeneza uvumi kwamba dawa hizo ni dawa za Virusi vya Corona, ambapo ameeleza kuwa Serikali ipo makini na kamwe haiwezi kuangamiza watu wake.

“Ndugu zangu dawa hizi ni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa watoto wetu wanajikinga na magonjwa ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele wakati mwingine wanaweza kukondeana nakupatwa na magonjwa mbalimbali kutokana na magonjwa ya minyoo ya tumbo na kichocho ,hali mabayo inaweza kupelekea mtoto kudumaa au kudumaza akili wataalamu wanasema inaweza hata kukusababishia kifo,” alisema Mahiba.

Shule ya msingi Iselamagazi yenye jumla ya wanafunzi 1,323 ambapo wanafunzi wote wenye umri wa kuanzia miaka mitano hadi 14 watapewa dawakinga hiyo.

DED Mahiba aliwaeleza wananchi wa halmashauri hiyo kuwa ili kudhibiti magonjwa hayo, wanapaswa kuzingatia watoto kuvaa viatu kwa kuwa kutovaa viatu ni njia hatarishi ya maambukizi hayo na kuwasisitiza walimu nao kuzingatia suala la usafi katika vyoo vinavyotiririsha hovyo maji machafu.

Kwa upande wake, Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kutoka hospitali ya wilaya - Iselamagazi, Dk. Charles Zacharia alisema kuwa wamelenga kutoa kingatiba hizo kwa wanafunzi 91,882 katika halmashauri hiyo, na wanatarajia kuendelea kutoa kingatiba kwa wanafunzi wote wenye sifa ili kuwakinga na magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo.

“Kwa ushirikiano wa walimu na wahudumu wa afaya waliopo zoezi litakwenda vizuri kama lilivyo agizo la serikali, niwaombe wazazi tuendelee kuruhusu watoto wetu waje kupata kinga na tiba hii muhimu sana,” alisema Dkt. Charles.

Awali Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Iselamagazi, Elias Lutubija ameeleza kuwa kabla ya zoezi la kuwapa kinga tiba, wanafunzi wote wamepewa chakula cha kutosha ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mwanafunzi kumeza dawa kabla ya kula chakula.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba (kulia) akimpatia dawa za kichocho na Minyoo ya tumbo mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Iselamagazi
Wanafunzi wa shule ya Iselamagazi katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakinywa dawa za kichocho na minyoo ya tumbo baada ya zoezi za ugawaji wa dawa hizo kuzinduliwa na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hoja Mahiba (kulia). Wa pili kushoto ni Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hapewi Kipaumbe halmashauri hiyo, Dk. Charles Zakaria
Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hapewi Kipaumbe halmashauri hiyo, Dk. Charles Zakaria akizungumza wakati wa kuzindua zoezi hilo
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Iselamagazi, Elias Lutubija akizungumza wakati wa kuzindua chanjo hiyo katika shule yake
Wanafunzi wa Shule ya msingi Iselamagazi wakiwa katika maandalizi ya kupata kinga tiba ya kichocho na minyoo ya tumbo

Picha na Shinyanga Press Club Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments