GARI LA MALIASILI LAUA WANAFUNZI WAWILI, KUJERUHI KAHAMA


Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wanafunzi wawili wa kidato cha nne katika shule ya Sekondari Isinuka iliyopo Wilayani Kahama wamefariki dunia na mmoja hali yake ni mbaya baada ya kugongwa na gari la Idara ya Maliasili Kahama wakitembea barabarani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP George Kyando ajali hiyo imetokea Juni 18, majira ya saa 09:30 katika eneo la Wigehe barabara ya Kahama Nyandekwa kata ya Zongomela Mjini Kahama.

“Gari yenye usajili namba STK 8768 aina ya Toyota Landcruiser mali ya Idara ya Maliasili Kahama ikiendeshwa na dereva Oscar Mwaliki (23) mkazi wa Bushushu Shinyanga akiwa anatokea Nyandekwa kuelekea Kahama aliwagonga watembea kwa miguu watatu ambao wote ni wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Isinuka iliyopo Wigehe wilayani Kahama”,ameeleza Kamanda Kyando.

"Ajali hiyo ilisababisha kifo cha Upendo Nicodem (18) mkazi Bukondamoyo papo hapo na Kiiza Ibrahimu (18),mkazi wa Wigehe ambaye amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza",ameongeza.

Amesema majeruhi Natalisi Sadoki (20) mkazi wa bukondamoyo aliyeumia kichwani anaendelea kupatiwa matibabu na kwamba hali yake ni mbaya.

Kamanda Kyando amesema chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendokasi uliopelekea tairi ya mbele kulia ya gari hilo kupasuka na kusababisha ajali hiyo.

Amesema dereva wa gari amekamatwa na gari iliyohusika kwenye ajali hiyo ipo katika kituo cha polisi Kahama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments