CHADEMA YATANGAZA KUTOSHIRIKI UCHAGUZI MDOGO WA MARUDIO KATA YA CHONA, JIMBO LA USHETU - SHINYANGA


Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi
****
TAARIFA KWA UMMA.

KUTOKUSHIRIKI UCHAGUZI MDOGO WA MARUDIO KATA YA CHONA, JIMBO LA USHETU - SHINYANGA.

Ndugu Wanahabari na Watanzania.
Tunapenda kuutaarifu umma kuwa, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga, hakitashiriki katika uchaguzi mdogo wa marudio, ambao umetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kufanyika Mwezi Julai, 2021 katika kata ya Chona, Halmashuri ya Ushetu. Mkoa wa Shinyanga.

Aidha, tunapenda kuutaarifu kuwa; mpaka sasa, Chama hakijafanya mchakato wowote wa ndani ya Chama (utoaji fomu, kura za maoni) na wala hakuna kikao chochote cha Kikatiba cha ngazi yoyote, kwa maana ya Kata wala Jimbo kilichoketi kupitisha Mgombea udiwani, katika Kata ya Chona kama ambavyo Katiba ya Chama ya mwaka 2006, Toleo la 2019, ibara ya 7.3.9 (a) na 7.4.10 (a) zinavyotaka.

Hata hivyo, tumepata taarifa za kushangaza kuwa kuna Mtu mmoja, ambaye hajulikani makazi wala anwani yake, ameghushi muhuri wa Chama, saini ya viongozi na kwenda kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea Udiwani kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata hiyo ya Chona.

Kwa hatua za awali, Chama tumekwisha kumuandikia barua rasmi Msimamizi Msaidizi wa Kata ya Chona, Barua yenye KUB CDM/USHT/01/2021.Pamoja na mambo mengine tumemtaka amuondoe mara moja Mtu huyo kwenye orodha na asitumie Jina na Nembo za CHADEMA . Kwa kuwa CHADEMA tumeazimia kutokushiriki Uchaguzi wowote wa marudio mpaka tutakapopata Tume Huru ya Uchaguzi Nchini.

Mwisho, Viongozi Mkoa na Taifa pamoja na Wanasheria wanafuatilia suala hili kwa uzito wake Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Pamoja na Salamu za Chama

Imetolewa leo 25.06.2021 na;
Emmanuel Ntobi
Mwenyekiti CHADEMA Mkoa Shinyanga



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments