WIZARA YA HABARI NA MALIASILI ZATAKIWA KUSHIRIKIANA KUTAMBUA MAENEO YA URITHI NA KUYALINDA

Na Shamimu Nyaki, Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana katika kuyatambua maeneo yanayokidhi vigezo vya kuingizwa katika Gazeti la Serikali na kuwa urithi wa Taifa ili yalindwe.

Mhe. Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Mei 21, 2021 Jijini Dar es Salaam alipofungua Kongamano la Kutambua na Kuenzi Mchango Anuwai wa Historia ya Tanzania katika Ukombozi wa Bara la Afrika, ambapo amewasisitiza Watanzania kujivunia historia hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na kulinda rasilimali za nchi kwa uzalendo, kuendelea kuwa na Utangamano,Utaifa pamoja na  kuenzi mazuri yaliyoachwa na wapigania Uhuru wa nchi na Afrika.

“Kongamano hili linaonyesha umuhimu wa Lugha ya Kiswahili katika Bara la Afrika kwa kuwa ndio lugha iliyotumika katika Harakati za ukombozi,nasisitiza Watanzania kutumia  Kiswahili ndani na nje ya nchi na lazima Wakalimani wengi wazalishwe ambao watasaidia kutafsiri lugha hii adhimu” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, ameendelea kusisitiza  umuhimu wa kufundishwa kwa Somo la Historia katika ngazi zote za shule lengo likiwa ni  kufundisha vijana historia ya Tanzania, umuhimu na mambo yote ambayo Tanzania imefanya ndani na nje ya nchi, kutambua umuhimu wa kulinda tunu na amali za nchi pamoja na umuhimu wa kuendelea kuilinda amani ya nchi.

Wakati huo huo Waziri Mkuu ametumia nafasi hiyo kuagiza Wizara ya Habari, TAMISEMI na Ofisi ya Rais kuchambua na kutolea maamuzi changamoto zinazowakabili Maafisa Michezo na Utamaduni ikiwemo ya Muundo wa Utumishi ili kila mmoja awajibike kilingana na Taaluma yake.

Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema Kongamano hilo  ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2011 ya kuwa Tanzania iwe na Makao Makuu ya Uhifadhi wa Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ili urithi huo usipotee kwa ajili ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

“Kongamano hili litaelimisha umma umuhimu wa kujikomboa kiuchumi na kifikra kupitia uhifadhi na utangazaji wa zao la utalii wa kiukombozi pamoja na kuhamasisha jamii kuwa na utangamano wa kitaifa ambao huzaa uzalendo”amesisitiza Mhe.Bashungwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa lengo la Kongamano hilo ni  kusherehekea mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Bara la Afrika, huku akieleza kuwa baada ya Kongamano hilo litafuatiwa na Kikao kazi kwa Maafisa Utamaduni na  Michezo kujadili mambo mbalimbali ya sekta hizo.

Katika Kongamano hilo Mada mbalimbali ikwemo  Mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Afrika na  Chimbuko la Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika na Umuhimu wake kwa Tanzania na Afrika,  pamoja na shuhuda mbalimbali za wapigania uhuru.

MWISHO..


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments