WAZIRI WA KILIMO AFUNGUA WARSHA YA KITAIFA JUU YA “KUTUMIA UWEKEZAJI MKUBWA KATIKA KILIMO KULETA MAENDELEO SHIRIKISHI TANZANIA”


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Tanzania inatambua umuhimu wa wakulima wote nchini – yaani wakulima wadogo, wa saizi ya kati na wakubwa - katika mageuzi ya kilimo na kuendeleza mbinu za kisasa na kilimo cha kibiashara chenye tija zaidi na faida kubwa  kwao.

Mkakati wa Sekta ya Kilimo (ASDS I na ASDS II) na Programu ya kuendeleza Kilimo (ASDP I na ASDP II) imelenga kukuza kilimo kwa ushirikiano baina ya Serikali na Sekta binafsi ili kuleta matumizi endelevu ya ardhi na maji, kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, huduma za utafiti na ughani, upatikanaji wa mbegu bora na pembejeo, masoko na uchakataji wa mazao ili kuongeza thamani za mauzo ya nje (value addition).

Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo Jijini Dodoma tarehe 21 Mei 2021 wakati akifungua warsha ya kitaifa juu ya “kutumia uwekezaji mkubwa katika kilimo kuleta maendeleo shirikishi tanzania” iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Kulingana na sera zetu za kilimo wawekezaji wakubwa wanategemewa sio tu kuzingatia haya katika kilimo chao wenyewe bali pia kusaidia wakulima wadogo – outgrowers na wakulima wengine - kwa kuwakopesha mbegu bora na pembejeo, kutoa elimu, ushauri na huduma za ughani kwa ujumla na kuingia mikataba mizuri ya kununua mazao yao” Amekaririwa Mhe Mkenda

Amesema kuwa Wakulima wakubwa wanategemewa pia kuchangia katika kuongeza thamani ya mazao na uboreshaji wa mnyororo wa thamani, na hivyo kuongeza bei za bidhaa za kilimo tunazouza nje ya nchi.

Amesema kuwa kunapokuwa na wawekezaji wakubwa na wa saizi ya kati ambao wengi wao huchukua maeneo makubwa ya ardhi, mojawapo ya majukumu ya serikali ni kulinda haki za raia na kuhakikisha ardhi yao na maji haviporwi, na pia wanalipwa fidia stahiki na bei nzuri kwa mazao yao.

Waziri Mkenda amesema kuwa Zaidi ya asilimia sabini (70%) ya watanzania wanaishi vijijini ambako wanajishughulisha na kilimo, kilimo huchangia 26%  hivi ya pato la taifa na asili mia thelathini (30%) ya mauzo ya nje (exports). “Lakini kwa miaka mingi tumejitahidi kuinua ubora wa kilimo kwa mafanikio japo si makubwa sana, kutokana na ujuzi mdogo wa wakulima wetu na matumizi hafifu ya sayansi na teknolojia ya kilimo, na hivyo tumeendelea kuwa na tija ndogo sana (low agricultural productivity) na upotevu wa mavuno” Amesema

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam/Taaluma Prof Bonaventure Rutinwa amesema kuwa Warsha hiyo ni kilele cha Utafiti wa mwaka mmoja uliofanywa na taasisi ya taaluma za maendeleo ya Chuo Kikuu cha dar es salaam kwa kushirikiana na Taasisi ya  Bill&Melinda Gates ikiwa na lengo la namna ya kutumia fursa za uwekezaji mkubwa katika kuchochea maendeleo katika sekta ya kilimo.

Naye, Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma ya Maendeleo Dkt Ronald Ndesanjo amesema kuwa radi huo wa utafiti ni sehemu ya majukumu ya taasisi hiyo ambapo ulikuwa na malengo makubwa mawili ikiwa ni pamoja na kufahamu kiwango cha ujumuishi katika ngazi ya miradi ya Uwekezaji wa kilimo chini ya Programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II).

Pia amesema lengo la pili ilikuwa ni kubuni namna bora ya kubadilisha mabadiliko jumuishi ya kilimo katika ngazi za uwekezaji pamoja na ngazi ya sera.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments