TMDA YAWAPIGA MSASA WAKAGUZI WA DAWA NA VIFAA TIBA SHINYANGA... RMO ATAKA UDHIBITI WIZI DAWA ZA SERIKALI

Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa dawa na vifaa tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Magharibi Dkt .Edga Mahundi, akizungumza kwenye mafunzo ya wakaguzi wa dawa na vifaa tiba mkoani Shinyanga.

Na Marco Maduhu, Shinyanga
MAMLAKA ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba hapa nchini (TMDA), imetoa mafunzo kwa wakaguzi wa dawa na vifaa tiba mkoani Shinyanga, namna ya kudhibiti matumizi holela ya bidhaa hizo, zikiwemo zisizosajiliwa, duni, bandia, pamoja na zilizomaliza muda wake.

Mafunzo hayo yamefanyika leo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kukutanisha wakaguzi hao dawa na vifaa tiba, kutoka Halmashauri zote za mkoa huo wakiwamo Wafamasia, Waratibu wa huduma za maabara na wataalamu wa mifugo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Meneja wa Mamlaka ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba (TMDA) kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi Dkt. Edga Mahundi, amewataka wakaguzi hao kuzingatia maadili wakati wa ukaguzi, kufuata sheria, kuacha jeuri, matusi, kejeli, pamoja na kutopokea Rushwa kwa watuhumiwa.

Amesema wakaguzi hao wakifanya kazi yao vizuri, hakutakuwa na uuzwaji wa madawa holela wala uingizwaji, yakiwemo maduka bubu na maabara, hali ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa nchi kuwa salama, pamoja na kulinda afya za wananchi kwa sababu ya kutotumia madawa yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu.

“Naombeni sana wakaguzi wa dawa na vifaa tiba mkoani Shinyanga, fanyeni kazi yenu kwa weledi ili kudibiti matumizi na uingizwaji wa dawa holela na vifaa tiba, sababu Mkoa huu unapakana na nchi jirani kwa upande wa Kahama, hivyo kuna hatari kubwa ya matumizi ya dawa zisizo sajiliwa, duni, bandia, pamoja na zilizomaliza muda wake,”amesema Mahundi.

“Dawa na vifaa tiba visivyo faa zikiingia hapa nchini, ni hasara kubwa kwa Serikali na kuathiri shughuli za uchumi sababu ya wananchi kuwa na afya duni, hivyo wakaguzi msiwe na mdhaha kwenye zoezi la ukaguzi,”ameongeza.

Kwa upande wake Mgeni rasmi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile, amewataka wakaguzi hao kudhibiti pia wizi wa madawa ya Serikali na kuuzwa kwenye maduka binafsi, huku zingine zikisafirishwa nchi jirani, au dawa za nje ya nchi kuingia hapa nchini zikiwa hazina usajili.

Pia alitoa mbinu kwa wakaguzi hao ili wapate kufanikiwa kudhibiti matumizi ya madawa holela na uingizwaji vikiwamo vifaa tiba, ni vyema wakafanya kazi karibu na viongozi wa Serikali za Mitaa, ili kuwapatia taarifa mbalimbali za watu ambao wanaihujumu Serikali yakiwamo na maduka bubu ya dawa na maabara.

TAZAMA PICH HAPA CHINI
Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa dawa na vifaa tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Magharibi Dkt Edga Mahundi, akizungumza kwenye mafunzo ya wakaguzi wa dawa na vifaa tiba mkoani Shinyanga.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile, akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba kutoka TMDA.
Washiriki wakiendelea na mafunzo.
Washiriki wakiendelea na mafunzo.
Mafunzo yakiendelea.
Picha ya pamoja ikipigwa na mgeni Rasmi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile katikati.

Na Marco Maduhu- Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments