DC AAGIZA MWALIMU AONDOLEWE WILAYA YAKE AKITUHUMIWA KUFANYA MAPENZI NA WANAFUNZI WATATU KITANDA KIMOJA

Mkuu wa  Wilaya  ya Magu mkoani Mwanza, Salim Kali, ameagiza kuhamishwa  wilayani kwake mwalimu anayetuhumiwa  kufanya mapenzi na wanafunzi watatu wa kike wa shule ya msingi ya Ilungu  katika kitanda kimoja.

Mwalimu huyo aliyetajwa na Mkuu wa wilaya kwa jina la Martin  Mambosasa anadaiwa kufanya vitendo hivyo kwa nyakati tofauti kwa miaka saba.

Mkuu huyo wa wilaya, alisema mwalimu huyo aliwahi kukamatwa na vyombo vya  dola na kufikishwa mahakamani, lakini akahonga wazazi wa watoto hao wakaharibu ushahidi.

Alitoa agizo hilo juzi kwenye kongamano la kuweka mikakati ya kukabiliana na ongezeko la vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, mimba katika umri  mdogo na utoro kwa wanafunzi.

Alisema  mikakati hiyo itasaidia  kuongeza ufaulu na kwamba  mwaka 2020, takwimu zinaonyesha matukio ya ukatili wa kijinsia yalikuwa 304.

Alimuagiza mratibu Elimu wa  kata na ofisa elimu wa wilaya kumhamishia mwalimu huyo  sehemu nyingine Ili asionekane wilayani kwake.

"Huyu mwalimu amekuwa akidhalilisha watoto wadogo kwa kipindi kirefu na naagiza ahamishwe sitaki kumsikia wala kumuona hapa wilayani kwangu," alisema

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa  Wilaya ya  Magu,  Amandus Mboya alisema  mambo yanayochangia ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia ni pamoja na wazazi kushindwa kuwapatia huduma muhimu.

Alitaja huduma zingine wanazokosa kuwa ni pamoja na kukosa taulo za kike, mafuta ya kupaka pamoja  na kukosa fedha za kunyoa nywele 

 

Credit:Nipashe




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments