DK. KALEMANI: UJENZI WA BWAWA LA UMEME JNHPP UMEFIKIA ASILIMIA 51.5

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa, utekelezaji wa mradi mkubwa wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere kwenye maeneo muhimu umefikia asilimia 51.5 kwa sasa.

Dkt. Kalemani ameyasema hayo Mei 22, 2021 alipokuwa kwenye ziara ya kukagua hatua za utekelezaji mradi huo wa Julius Nyerere akiambatana na Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutoka Misri, Dkt. Assem Elgazzar.

Dkt. Kalemani ameyataja maeneo ya ujenzi huo yaliyokamilika kwa asilimia hizo kwa ujumla wake kuwa ni, ujenzi wa tuta kuu, ujenzi wa wa jumba la kuendeshea mitambo, ujenzi wa njia za kupeleka maji kwenye mitambo ya kufua umeme pamoja na kituo cha kupokea na kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400.

“Mbali ya utekelezaji wa mradi kufika hatua hiyo lakini pia hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa shilingi trilioni 2.4 kulingana na mpango kazi” amesema Dkt. Kalemani.

Katika hatua nyingine transfoma sita kati ya ishirini na saba zitakazofungwa kwenye kituo cha kupokea umeme zimewasili, ambapo Dkt. Kalemani ameiagiza ziharakishwe kutolewa Bandarini na kupelekwa eneo la mradi ili kazi ya kuzifunga ianze.

Kwa upande wake Waziri wa Nyumba na Makazi kutoka Misri Dkt. Assem Elgazzar amesema kuwa, Serikali ya Misri inaendelea kuusimamia mradi na kuahidi utakamilika kwa wakati mwezi Juni 2022 kama ilivyo kwenye mkataba.

Awali akielezea maendeleo ya utekelezaji wa mradi kwa niaba ya Mhandisi Mkazi, Mhandisi Lutengano Mwandambo kutoka TECU amesema timu ya wataalamu kutoka Tanzania imeenda kukagua utengenezaji wa mitambo ya kufua umeme itakayotumika katika mradi huo.

Aliongeza kuwa, kufikia mwezi Novemba mwaka huu kazi ya kujaza maji kwenye bwawa itaanza ambapo itakwenda hadi Aprili mwaka 2022 ambapo kiwango cha maji kitakuwa kimefikia kina cha 163 juu ya usawa wa bahari, kiwango ambacho kinatosha kuanza kufua umeme.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments