TBS YATOA ELIMU YA VIWANGO KWA WANAFUNZI 15,526 WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI NA WANANCHI 12,250


Wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari 15,526 na wananchi 12,250 wanaoendesha shughuli zao kwenye maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu,  kama stendi, kwenye masoko, minada,magulio katika maeneo mbalimbali ya Wilaya za Kilosa, mkoani Morogoro, Bagamoyo mkoani Pwani  na Mkinga,  Tanga wamepewa elimu kuhusiana na umuhimu wa kutumia bidhaa zilizothibitishwa ubora na kusajiliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) .

Kampeni hiyo ya elimu kwa umma ilianza kutolewa maeneo mbalimbali ya wilaya za Kilosa, Bagamoyo na Mkinga na maofisa wa TBS  kuanzia Mei 4 hadi mwishoni mwa wiki hii.

Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Uhusiano wa TBS, Neema Mtemvu, alisema kitu kikubwa ambacho wamekifanya ni kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari juu ya umuhimu wa kutumia bidhaa zilizothibitishwa na kusajiliwa na TBS,majukumu ya shirika ikiwa ni pamoja na kuwapa namba ya mawasiliano kwa ajili ya kupiga bure kuwasiliana na shirika hilo pindi ikitokea wakapata matatizo  au changamoto kwenye bidhaa.

Alisema wamefikisha elimu hiyo kwa wanafunzi kwa kutambua kwamba wataenda kuwa mabalozi wazuri kwa wazazi na walezi kuhusiana na umuhimu wa kutumia bidhaa zilizothibitishwa na TBS.

Kwa upande wa maeneo yenye mikusanyiko ya watu, Mtemvu alisema elimu hiyo imetolewa Mkinga katika Stendi  ya Hororo na gulio la Duga, huku kwa upande wa Kilosa  elimu hiyo ikitolewa Uhindini, Sabasaba na Kimamba.

Aidha elimu hiyo ilitolewa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Bagamoyo katika stendi ya Bagamoyo na soko la toptop ambako ilihitimishwa katika wilaya hizo tatu.

Kuhusu mwitikio wa wananchi katika maeneo hayo yenye mikusanyiko ya watu, Mtemvu alisema wengi wamefurahishwa na elimu hiyo na wameomba iwe endelevu .

"Wananchi wameshukuru shirika kwa kuona umuhimu wa kuwapatia taarifa hizo kuhusu viwango  kwa sababu wamekuwa wakipata changamoto kubwa, lakini walikuwa hawajui wafanyeje.

Lakini kwa sasa na wenyewe wameahidi kuingia kwenye vita ya bidhaa hafifu kwa sababu wana uwezo wa kuwasiliana na TBS, kwani wanajua tupo," alifafanua Mtemvu.

Alisema miongoni mwa mambo walioelimishwa wananchi hao kupitia kampeni hiyo ni pamoja na majukumu ya TBS,  umuhimu ya kuangalia tarehe ya mwisho ya matumizi ya bidhaa wanazotaka kununua, ambapo taarifa hizo zinapatikana kwenye vifungashio.

Eneo lingine ambalo wananchi hao walielimishwa ni umuhimu wa wao kununua bidhaa zilizothibitishwa na kusajiliwa na TBS. Mtemvu alitaja baadhi ya faida za kununua bidhaa zilizothibitishwa na shirika hilo kuwa ni pamoja na kulinda afya zao na thamani za fedha zao.

Alisema mtu anaponunua bidhaa ambazo zimethibitishwa na TBS anakuwa na uhakika na bidhaa anazozitumia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments