Breaking : SERIKALI YATANGAZA NAFASI ZA AJIRA...UALIMU, AFYA... KUOMBA MWISHO MEI 23

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu akitangaza ajira za walimu 6949 wa shule za msingi na sekondari katika mkutano wake na waandishi wa habari (hawapo pichani) uliofanyika Mei 09, 2021 jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu akitangaza ajira za walimu 6949 wa shule za msingi na sekondari katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Mei 09, 2021 jijini Dodoma. Pembeni yake ni Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Gerald Mweli.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama akiwa katika mkutano wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI na waandishi wa habari uliofanyika Mei 09, 2021 jijini Dodoma.

Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, anayesimamia Elimu ya Awali na Msingi, ambaye pia ni Kamishna wa TSC, Susan Nussu, akiwa katika mkutano wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI na waandishi wa habari uliofanyika Mei 09, 2021 jijini Dodoma.

**********************

Na Adili Mhina.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu ametangaza nafasi za ajira za walimu 6,949 wa Shule za Msingi na Sekondari zinazolenga kujaza nafasi wazi za watumishi waliokoma utumishi wao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo, kuacha kazi, kufukuzwa kwenye utumishi na kustaafu.

Waziri Ummy alitoa kauli hiyo leo Mei 9, 2021 wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za TAMISEMI jijini Dodoma kwa lengo la kutoa taarifa ya ofisi yake kupata kibali cha ajira kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

“Tumepata kibali cha ajira za walimu 6,949 pamoja na watumishi 2,726 wa Kada ya Afya. Hivyo, nachukua fursa hii kuutangazia umma kuwa taratibu za kuanza mchakato wa kuomba ajira hizo umekamilika na kwamba waombaji wote wenye nia ya kuomba, sasa wanaweza kufanya hivyo”, alisema.

Alifafanua kuwa waombaji wanatakiwa kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia kiunganishi ajira.tamisemi.go.tz kuanzia Mei 09 hadi 23 mwaka huu.

Hata hivyo, alieleza kuwa kwa upande wa watu wenye ulemavu hawatalazimika kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao badala yake watatuma maombi yao yakiwa katika nakala ngumu.

“Kwa ndugu zetu wenye ulemavu wanaweza kutuma maombi yao kwa nakala ngumu. Maombi hayo yaeleze aina ya ulemavu na yaambatane na picha kisha yatumwe kwa Katibu Mkuu TAMISEMI. Nakala ya Maombi hayo itumwe Ofisi ya Waziri Mkuu ili Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu wenye Ulemavu aione.

Waziri Ummy alisema Ofisi yake imebainisha sifa mbalimbali za kitaaluma ambazo waombaji wanapaswa kuwa nazo kulingana na muundo wa kada ya ualimu wa shule za msingi na sekondari nchini.

Akianza kueleza sifa za zinazotakiwa kwa walimu wa shule za msingizi, Waziri Ummy alisema katika nafasi ya Mwalimu Daraja IIIA, mwombaji anatakiwa kuwa mhitimu wa Astashahada ya Ualimu Elimu ya Msingi, Astashahada ya Ualimu Elimu ya Michezo, Astashahada ya Ualimu Elimu ya Awali na Astashahada ya Ualimu wa Elimu Maalum.

Aliongeza kuwa mwalimu Daraja la IIIB anatakiwa mhitimu mwenye Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Awali, Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Msingi na Stashahada ya Ualimu wa Elimu Maalum.

Vilevile, alisema kuwa katika nafasi ya Mwalimu Daraja la IIIC anatakiwa mhitimu mwenye Shahada ya Ualimu katika masomo ya “English Language, History na Geography”.

Kwa Upande wa shule za sekondari, Ummy alifafanua kuwa nafasi ya Mwalimu Daraja la IIIB inahitaji mhitimu wa Stashahada ya Ualimu wa masomo ya “Physics, Mathematics, Biology na Chemistry”.

Pia, katika nafasi ya Mwalimu Daraja la IIIC mwombaji anatakiwa kuwa na sifa mojawapo kati ya Shahada ya Ualimu, Shahada ya Elimu Maalum na Stashahada ya Uzamili katika Elimu (Post Graduate Diploma in Education) katika masomo ya “Physics, Chemistry, Biology na Mathematics”.

Waziri ummy aliongeza kuwa kwa waombaji waliopata elimu Nje ya Nchi, wanatakiwa kuzingatia taratibu zilizowekwa za kupata uthibitisho wa elimu zao kwa mamlaka zinazohusika kabla ya kuomba ajira hizo.

“Waombaji wote waliosoma Elimu ya Sekondari Nje ya Nchi wanatakiwa kupata namba ya ulinganifu wa matokeo kutoka Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA). Waombaji waliosoma Vyuo Nje ya Nchi wanatakiwa kupata Ithibati ya masomo yao kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Ummy alisisitiza kuwa kila mwombaji ni lazima awe Raia wa Tanzania mwenye umri usiozidi miaka 45, awe na namba ya kitambulisho cha Taifa, awe na vyeti kamili vya mafuzo ya fani aliyosomea na asiwe mwajiriwa wa Serikali au aliyewahi kuajiriwa na Serikali.

Mkutano huo wa Waziri na Waandishi wa Habari ulihudhuriwa na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama ambaye Ofisi yake ndiyo Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa walimu wa shule za masingi na sekondari walioajiriwa katika utumishi wa Umma.


*********

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR -TAMISEMI) imepata kibali cha ajira za Watumishi wa Kada mbalimbali za Afya 2,726 kwa ajili ya Hospitali za Halmashauri, Vituo vya Afya na Zahanati pamoja na Walimu 6,949 wa Shule za Msingi na Sekondari watakaofanya kazi chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.

Kwa sababu hiyo, wahitimu kutoka kwenye Vyuo vya Elimu ya Juu, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Afya vinavyotambuliwa na Serikali wanatangaziwa kutuma maombi yao ya nafasi za kazi kuanzia tarehe 09-23 Mei, 2021.

Nafasi za ajira zilizopo ni kwa wahitimu wa Astashahada (Certificate), Stashahada (Diploma) na Shahada (Degree). 

A: TARATIBU ZA KUOMBA AJIRA ZA UALIMU

Walimu wote wenye sifa watume maombi kwa njia ya mtandao kupitia kiunganishi cha ajira.tamisemi.go.tz kwa utaratibu ufuatao:

-i.Walimu wote wenye sifa ambao hawakuomba ajira za ualimu (tarehe 07.09.2021) watume maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia kiunganishi cha ajira.tamisemi.go.tz;

ii.Walimu walioomba ajira kwa njia ya mtandao kufuatia Tangazo la Ajira la tarehe 07 Septemba, 2020, wanaelekezwa kuingia kwenye akaunti zao walizotumia wakati wa kutuma maombi ili kuhakiki usahihi wa taarifa na viambatisho walivyotuma hapo awali; na

iii.Tangazo hili linawahusu wahitimu wa Kozi za Ualimu kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2019.

2.0 SIFA ZA WAOMBAJI

2.1SIFA ZA KITAALUMA ZA MWOMBA JI

Walimu wanaotakiwa kutuma maombi wawe na Sifa za kitaaluma kama ifuatavyo:

2.1.1 WALIMU WA SHULE ZA MSINGI

Walimu wanaoomba kuajiriwa kufundisha Shule za Msingi wawe na Sifa zifuatazo:

i.Mwalimu Daraja la III

A: Mhitimu wa Astashahada ya Ualimu Elimu ya Msingi, Astashahada ya Ualimu Elimu ya Michezo, Astashahada ya Ualimu Elimu ya Awali na Astashahada ya Ualimu wa Elimu Maalum;

ii.Mwalimu Daraja la III

B:Mhitimu wa Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Awali, Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Msingi na Stashahada ya Ualimu wa Elimu Maalum;na iii.Mwalimu Daraja la III

C:Mhitimu wa Shahada ya Ualimu katika masomo ya “English Language, History na Geography”.

2.1.2 WALIMU WA SHULE ZA SEKONDARI

i.Mwalimu Daraja la III

B:Mhitimu wa Stashahada ya Ualimu wa Masomo ya “Physics, Mathematics, Biology na Chemistry”;ii.Mwalimu Daraja la IIIC:Mhitimu wa Shahada ya Ualimu aliyesomea Elimu Maalum kwa Masomoya “Physics, Chemistry, Biology naMathematics”;

iii.Mwalimu Daraja la IIIC:Mhitimu wa Shahada ya Ualimu wa Masomo ya “Physics, Mathematics, Chemistry na Biology”; naiv.Mwalimu Daraja la IIIC:Mhitimu wa Stashahada ya Uzamili katika Elimu (Post Graduate Diploma in Education) lazima awe mwenye Shahada ya Kwanza (Bachelor Degree) yenye Masomo yaliyotajwa katika (ii) na iii) hapo juu.

2.2. WAHITIMU WALIOSOMA NJE YA NCHI

i.Waombaji wote waliosoma Elimu ya Sekondari nje ya nchi wanatakiwa kupata Namba ya Ulinganifu wa Matokeo (Equivalent Number) inayoanza na Herufi EQ...kutoka Baraza la Mitihani la Tanzania ili kuwawezesha kuingia kwenye Mfumo wa Ajira; na

ii.Waombaji waliosoma Vyuo Nje ya Nchi wanatakiwa kupata Ithibati ya masomo yao kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili vyeti vyao viweze kutambuliwa na kupata uhalali wa kutumika hapa nchini.

3.0 SIFA ZA JUMLA ZA MWOMBAJI WA AJIRA ZA UALIMU

Mwombaji wa nafasi zilizoainishwa hapo juu awe na sifa za jumla zifuatazo:

-i.Awe ni Mtanzania;

ii.Awe na umri usiozidi miaka arobaini na tano (45);

iii.Awe hajawahi kufukuzwa, kuacha kazi au kustaafishwa katika Utumishi wa Umma;

iv.Awe na namba ya kitambulisho cha Taifa;

v.Waombaji wenye Shahada na Stashahada za NACTE na TCU (UDOM) waambatishe Cheti cha Kuhitimu Mafunzo na “Transcript”.

Waombaji wa Astashahada na Stashahada za NECTA waambatishe Cheti cha Mafunzo katika sehemu mbili (weka cheti na weka “transcript”);

vi.Nakala ya Cheti cha Kidato cha Nnena Sita; vii.Nakala ya Cheti cha Kuzaliwa;naviii.Maelezo Binafsi (CV), yakionesha umri, anuani kamili na namba ya simu ya kiganjani.

B:TARATIBU ZA KUOMBA AJIRA KADA ZA AFYA

Wataalamu wa Kada za Afya wenye sifa watume maombi kwa njia ya mtandao kupitia kiunganishi cha ajira.tamisemi.go.tz: -2.0

Sifa za Waombaji ni kama ifuatavyo:-

2.1DAKTARI DARAJA LA II

Waombaji wawe na Shahada ya Udaktari wa Binadamu kutoka Vyuo Vikuu/Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali waliomaliza Mafunzo ya Kazi “Internship” ya muda usiopungua mwaka mmoja na kupata Usajili kutoka Baraza la Madaktari Tanganyika (Medical Council of Tanganyika).

2.2 DAKTARI WA MENO DARAJA LA II

Waombaji wawe na Shahada ya Udaktari wa Binadamu kutoka Vyuo Vikuu/Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali waliomaliza Mafunzo ya Kazi “Internship” ya muda usiopungua mwaka mmoja na kupata Usajili kutoka Baraza la Madaktari Tanganyika (Medical Council of Tanganyika).

2.3 TABIBU DARAJA LA II

Waombaji wawe na Stashahada ya Utabibu (Diploma in Clinical Medicine) ya muda wa miaka mitatu kutoka Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali.

2.4 TABIBU MSAIDIZI

Waombaji wawe wamehitimu Astashahada ya miaka miwili ya Tabibu Wasaidizi (Clinical Assistants Certificate) kutoka Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali.

2.5 TABIBU WA MENO DARAJA LA II Waombaji wawe na Stashahada ya Tabibu Meno (Diploma in Clinical Dentistry) ya muda wa miaka mitatu kutoka Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali.

5.6TABIBU MENO MSAIDIZI

Waombaji wawe wamehitimu Astashahada ya miaka miwili ya Tabibu Wasaidizi (Clinical Assistants Certificate) kutoka Chuo kinachotambuliwa na Serikali.

2.7 MFAMASIA DARAJA LA II

Waombaji wawe na Shahada ya Famasi kutoka Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali waliohitimu Mafunzo kwa Vitendo (Internship) ya mwaka mmoja na ambao wamesajiliwa na Baraza la Famasi (Pharmacy Council).

2.8 MTEKNOLOJIA (DAWA) DARAJA II

Waombaji wawe na Stashahada katika fani ya Uteknolojia wa Dawa (Diploma in Pharmaceutical Technology) kwa muda wa miaka mitatu kutoka Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali na ambao wamesajiliwa na Baraza la Famasi (Pharmacy Council).

2.9 MTEKNOLOJIA MSAIDIZI (DAWA)

Waombaji wawe na Astashahada katika fani ya Uteknolojia wa Dawa ya Afya (Certificate in Pharmaceutical Technology) kwa muda wa miaka miwili kutoka Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali na ambao wamesajiliwa na Baraza la Famasi (Pharmacy Council).

2.10 MTEKNOLOJIA (MAABARA) DARAJA II

Waombaji wawe na Stashahada katika fani ya Uteknolojia wa Maabara ya Afya (Diploma in Health Laboratory Sciences) kwa muda wa miaka mitatu kutoka Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali na ambao wamesajiliwa na Baraza la Wataalamu wa Maabara za Afya (Health Laboratory Practitioners’ Council).

2.11MTEKNOLOJIA MSAIDIZI (MAABARA)

Waombaji wawe na Astashahada katika fani ya Uteknolojia wa Maabara ya Afya (Certificate in Health Laboratory Sciences) kwa muda wa miaka miwili kutoka Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali na ambao wamesajiliwa na Baraza la Wataalamu wa Maabara za Afya (Health Laboratory Practitioners’ Council).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments