WAZIRI BASHUNGWA : TUNAFUATILIA TUKIO LA WAANDISHI WA HABARI KUWEKWA CHINI YA ULINZI NA MKURUGENZI MANISPAA YA TEMEKE

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inafuatilia malalamiko ya wadau wa Tasnia ya Habari juu ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Lusabilo Mwakabibi,kuweka chini ya ulinzi Waandishi wa habari jana Aprili 12,2021 jijini Dar es salaam.

"Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo tunafuatilia malalamiko ya wadau wa Tasnia ya Habari juu ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Ndugu Lusabilo Mwakabibi, kuweka chini ya ulinzi Wanahabari, tunaomba Wanahabari wawe na subira wakati allegations hizi za kusikitisha zinafanyiwa kazi”, ameandika Waziri Bashungwa kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Twitter.

Mapema jana taarifa zilisambaa mtandaoni kuhusu Waandishi wa habari Christopher James wa ITV & Radio One na Dickson Billikwija wa Island Tv kuwekwa chini ya Ulinzi wa Polisi takribani saa tatu kwa Maagizo ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Lusabilo Mwakabibi.

Inaelezwa kuwa kulikuwa na kikao ambacho Mkurugenzi alikiitisha na wafanyabiashara kutoka Soko la Mbagala Rangi Tatu kisha wafanyabiashara hao waliwaita Wanahabari hao ambao walifika hapo kutekeleza majukumu yao kitendo ambacho huenda kilimkera Mkurugenzi huyo ambapo aliwaamuru askari wao wawaweke chini ya ulinzi mpaka wamalize kikao kwa hatua zaidi.

Taarifa za Mkurugenzi kuzuia waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao zimezua mjadala mtandaoni na kwenye vyombo vya habari ambao wengi wamekuwa wakihoji mkurugenzi huyo anatumia mamlaka yapi kuzuia waandishi kutekeleza majukumu yake huku ikidaiwa kuwa siyo mara yake ya kwanza kukwazana na waandishi wa habari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments