HER INITIATIVE YAZINDUA JUKWAA LA PANDA DIGITAL LENYE LENGO LA KUWAJENGEA UWEZO NA KUWAPATIA WASICHANA UJUZI NA FURSA ZA UJASIRIAMALI


Shirika la Her Initiative kwa kushirikiana na kampuni ya Serengeti Bytes limezindua jukwaa la kidigitali la kwanza la kiswahili lenye lengo la kuwasaidia wasichana kupata ujuzi na rasilimali za kuanza na kuendesha biashara zao ili kufikia malengo ya kujikwamua kiuchumi. 

Jukwaa hili linafahamika kama Panda Digital likiwa na maana ya kupanda mbegu ya kujitegemea kiuchumi kwa kupitia majukwaa ya kidigitali. Jukwaa hili linawaleta pamoja wasichana wajasiriamali popote walipo Tanzania na kuwajengea uwezo pamoja na kuwapa ujuzi wa masuala mtambuka wa biashara na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za ufadhili, mitaji na mikopo zilizopo katika taasisi binafsi na za serikali.

Jukwaa la Panda digital limeanzishwa kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwapatia wasichana ujuzi utakaowasaidia kutengeza kipato kwa kuanzisha na kuendesha biashara, kuchochea ushiriki wa wanawake vijana katika uchumi wa kidigitali, kuwaunganisha wasichana na fursa za kifedha kama mitaji, mikopo, ufadhili, kuhamasisha uvumbuzi na ubunifu miongoni mwa wasichana na kuhakikisha wasichana wana uhakika wa kuongeza ujuzi wa kukabiliana na changamoto kibiashara hasa katika kipindi cha majanga kama COVID 19.

Vilevile jukwaa la Panda Digital linatarajiwa kuwa kanzidata maalumu ya wasichana na wanawake wajasiriamali kutoka mikoa yote ya Tanzania. Pia, Panda Digital itakuwa jukwaa la wasichana wajasiriamali kutangaza bidhaa na/au huduma zao kupitia kipengele maalumu kinachofahamika kama Soko. 

Katika jukwaa hili kutakuwa na kozi mbalimbali za kuongeza ujuzi wa kibiashara kama kozi za masoko mtandaoni, huduma kwa wateja, namna ya kutengeneza chapa ya biashara na namna ya kufanya ufungashaji na masuala mengine kama namna ya kukabiliana na changamoto za kibiashara. 

Kwa sasa kozi iliyokamilika ni kozi ya masoko mtandaoni na tayari imewekwa kwenye jukwaa la Panda Digital kwa ajili ya matumizi. Kozi ya masoko mtandaoni ina masomo 12 na sehemu ya maswali na majibu iliyoambatanishwa kila baada ya kumaliza somo moja lengo ni kuwasaidia wajasiriamali kupata uelewa zaidi.

Namna ya kutumia jukwaa la Panda Digital, tembelea tovuti pandadigital.co.tz, bonyeza kitufe cha usajili, fuata maelekezo yaliyoorodheshwa kwenye jukwaa, utapokea ujumbe mfupi wenye kiunzi cha kuthibitisha usajili wako kupitia barua. Ukishakamilisha usajili, utaingia moja kwa moja na kupelekwa ukurasa wa nyumbani. Baada ya kufanikiwa kujisajili, utaona kitufe kilichoandikwa kozi. 

Ukibonyeza utapelekwa moja kwa moja eneo ambalo kozi zimeorodheshwa. Bonyeza kozi unayoipenda na ruhusu kitufe cha Anza Mafunzo. Baada ya kumaliza kozi utapata cheti. 

Kupitia jukwaa la Panda Digital wajasiriamali wasichana na wanawake wanaweza kupata fursa mbalimbali za kibiashara kwa kubonyeza kitufe kilichoandikwa fursa ambapo wanaweza kupata fursa za ufadhili na mafunzo megine yaliyowekwa kulingana na mahitaji yako.

“Jukwaa la Panda Digital linalenga kupunguza pengo la matumizi ya kidigitali kati ya wanawake na wanaume kwa kuchochea ushiriki wa wanawake ili kutengeneza kipato katika uchumi wa digitali.

 Jukwaa hili pia linaondoa vikwazo vya muda, rasilimali, umbali kwa kuhakikisha wasichana na wanawake wajasiriamali wanapata ujuzi popote walipo na pia wanaweza kupata ujuzi na kuunganishwa na fursa mbalimbali za kukuza biashara zao”, Lydia Charles Moyo Mkurugenzi wa Her Initiative.

Jukwaa la Panda Digital limeandaliwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Serengeti Bytes, Mtabe na Women First International Fund.

Kuhusu Her Initiative
Her Initiative ni Shirika lisilo la kiserikali lenye lengo la kuwaimarisha wasichana kiuchumi kwa kuvunja duara la umasikini na kujenga ustahimilivu wa kiuchumi. Her Initiative inawajengea uwez, inawapa wasichana maarifa, ujuzi na rasilimali za kuwasaidia kutengeneza kipato chao wenyewe. Kupitia kazi zetu tunahamasisha ushiriki wa wasichana katika masuala ya kiuchumi ili kufikia usawa wa kijinsia na uchumi jumuishi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments