RAIS WA CHAD AUAWA KWA KUSHAMBULIWA NA WAASI | MALUNDE 1 BLOG

Tuesday, April 20, 2021

RAIS WA CHAD AUAWA KWA KUSHAMBULIWA NA WAASI

  Malunde       Tuesday, April 20, 2021

Jeshi la Chad limetangaza kuwa Rais wa nchi hiyo Idriss Deby (68)amefariki baada ya kupata majeraha kwenye mapambano dhidi ya waasi.

Deby alienda mstari wa mbele mwishoni mwa wiki kuvitembelea vikosi vya nchi hiyo ambavyo vinapambana na waasi kaskazini mwa nchi hiyo. Waasi hao wamevuka mpaka wakitokea Libya.

Kifo chake kimetokea ikiwa ni saa chache tu tangu matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanyika Aprili 11 kuonesha kuwa anaongoza kwa asilimia 80. Kwa ushindi huo, Deby angeiongoza nchi hiyo kwa awamu ya sita mfululizo.

Serikali na bunge vimevunjwa na sasa baraza la kijeshi ndilo litakaloiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miezi 18 ijayo.

Bw. Déby aliingia madarakani mwaka 1990 baada ya mapinduzi ya kijeshi.

Waasi hao kutoka kundi linalojiita Fact (the Front for Change and Concord in Chad), walishambulia kitua cha mpaka wa Libya na Chad siku ya uchaguzi, yaani Aprili 11. Walikuwa wakisonga mbele kuelekea mji mkuu wa N'Djamena.

Kundi hilo la waasi liliundwa na maafisa wa jeshi walioasi mwaka 2016 wakimshutumu Rais Deby kwa kuminya haki za watu siku chache kabla ya uchaguzi. Waasi hao wakakita kambi katika milima ya Tibesti ambayo inatengeneza sehemu ya mpaka wa Chad na Libya.

Mapambano baina ya waasi na wanajeshi wa serikali yaliaza siku ya Jumamosi. Jenerali wa jeshi ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa waasi 300 waliuawa na wengine 150 kukamatwa katika mapambano hayo. Aliongeza kuwa jeshi lilipoteza askari watano na wengine 36 wakijeruhiwa. Hata hivyo idadi hiyo haikuweza kuthibitishwa mara moja.

Jeshi limetangaza marufuku ya kutoka nje wakati wa usiku, kuanzia saa 12 jioni mpaka saa 11 alfajiri kuanzia leo. Pia mipaka yote ya nchi hiyo ikiwemo anga imefungwa.

Baadhi ya balozi zimeshauri wafanyakazi wake kuondoka katika mji mkuu huo.

Bw. Déby kwa muda mrefu amekuwa mshirika mkubwa wa Ufaransa na mataifa mengine ya magharibi. Hata hivyo kumekuwa na ongezeko la ukosoaji ndani ya nchi kwa namna ambavyo serikali yake ilikuwa ikitumia mapato yatokanayo na mauzo ya mafuta.

Wakati wa kampeni za uchaguzi, aliahidi kuboresha amani na ulinzi katika ukanda huo.

'Mtoto wa Deby kuongoza nchi'

Shirika la habari la kimataifa la AFP linamnukuu msemaji wa jeshi kuwa mtoto wa rais aliyeuawa ndiye atakayeliongoza baraza la kijeshi linaloiongoza nchi hiyo.

Mtoto huyo, Mahamat Idriss Deby, 37, ni manajeshi wa cheo cha juu cha jenerali.

Baba yake pia alikuwa mwanajeshi, na alisifika ndani na nje ya nchi kwa harakati zake za kupambana na waasi.


Takriban mwaka mmoja uliopita, aliongoza mapambano mstari wa mbele ambapo inaripotiwa wanamgambo 1,000 wa Boko Haram waliuawa. Mwaka jana pia alipewa cheo cha juu zaidi cha kijeshi cha Field Marshall kutokana na harakati zake hizo.

Japo baadhi ya watu wanasema ni jambo lilisilo la kawaida kwa Rais kuwa mstari wa mbele vitani, mwandishi wa BBC Beverly Ochieng anaripoti kuwa Rais Idriss Déby alikuwa mwanajeshi wa cheo cha juu cha field marshal na ilikuwa ni jambo la kawaida kwake kuwa mstari wa mbele na wanajeshi wake.

Takribani mwaka mmoja uliopita, Déby aliongoza operesheni ya kijeshi akiwa mstari wa mbele na inaripotiwa wanamgambo 1,000 wa Boko Haram waliuawa katika mapambano hayo.

Alipokea mafunzo ya kijeshi nchini Ufaransa na kufuzu kama rubani wa ndege vita.

Déby alikuwa afisa wa jeshi wa cheo cha juu aliporatibu mapinduzi yaliyomng'oa madarakani rais Hissène Habré mwaka 1990. Toka hapo Deby akachukua hatamu za uongozi mpaka umauti ulipomkuta, akiwa vitani.

CHANZO - BBC SWAHILI


Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post