KAMPUNI YA ISRAEL YAANZA MAZUNGUMZO YA AWALI YA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA MIFUGO NCHINI


Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amekutana na kufanya mazungumzo ya awali na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Smart Holding ya nchini Israel Bw. Avi Postelnik yenye lengo la kuwekeza hapa nchini kupitia sekta mbalimbali zikiwemo za mifugo na uvuvi.

Akizungumza jana (16.04.2021) mara baada ya kuhitimisha mazungumzo yao ya awali katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es Salaam, Prof. Gabriel amesema katika mazungumzo yao wameainisha fursa kubwa zilizopo hapa nchini ikiwemo ya unenepeshaji mifugo na uongezaji thamani wa bidhaa zitokanazo na mazao ya mifugo.

Amesema nchi ya Israel ina ng’ombe ambao wana uwezo wa kutoa lita 40 hadi 50 za maziwa kwa siku moja na kwamba Bw. Postelnik amewaona ng’ombe wa aina hiyo hapa nchini katika Mkoa wa Kagera.

“Kwa bahati nzuri tayari kosaafu hiyo ya ng’ombe ameiona hapa Tanzania katika Mkoa wa Kagera na tuna dume la ng’ombe kutoka nchini Israel, ambalo lipo katika Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) kilichopo Mkoani Arusha.” Amefafanua Prof. Gabriel

Aidha, ameongeza kuwa mkakati mzuri ukiwekwa baina ya Tanzania na Israel katika kukuza sekta ya mifugo hapa nchini, wafugaji wanaweza kupata faida kubwa hasa baada ya Israel kuwa na teknolojia ya kutengeneza malisho ya mifugo kwa kutumia mabaki ya mazao ya mifugo.

Katika mazungumzo hayo wamegusia umuhimu wa masoko ya bidhaa za mifugo na uvuvi, ambapo wamekubaliana kuwa na masoko ya bidhaa za mifugo na uvuvi katika nchi mbalimbali kutatoa hamasa zaidi kwa wafugaji na wavuvi kuzalisha zaidi bidhaa zao.

Katika mazungumzo hayo ya awali ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Smart Holding ya nchini Israel Bw. Avi Postelnik wamesema eneo ambalo wanalipa kipaumbele kwa sasa katika sekta ya mifugo ni ufugaji wa ng’ombe na uzalishaji wa mazao yatokanayo na ng’ombe ukifuatiwa na ufugaji wa kuku.

MWISHO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments