TBS YAFANYA UKAGUZI WA KUSHTUKIZA KANDA YA MAGHARIBI KWENYE MADUKA YA VYAKULA NA VIPODOZI

Wakaguzi wa TBS wakiendelea na ukaguzi na usajili wa majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi Mkoani Pwani. TBS inawakumbusha wauzaji na waagizaji wa bidhaa hizo kuhakikisha wanasajili ili kuhakiki ubora na usalama wake ili kuepuka usumbufu usio wa lazima sambamba na kuzingatia taarifa muhimu kwenye bidhaa husika kama vile muda wa matumizi na orodha ya viambata.
Mkaguzi wa TBS, Bw. Elisha Meshack akimfanyia usajili mmiliki wa duka la chakula mara baada ya ukaguzi wa duka lake wilayani Kakonko. TBS inawakumbusha wenye majengo ya chakula na vipodozi kufanya usajili mara moja ili kuepuka usumbufu
 Mmiliki wa duka la chakula na vipodozi wilayani Kakonko akionesha vibali vyao vya majengo kwa wakaguzi wa TBS wakati wa ukaguzi wa kushtukiza sokoni na usajili wa majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi. TBS inawakumbusha wenye majengo hayo kusajili ili kuepuka usumbufu
Mkaguzi wa TBS, Bw. Emmanuel Mushi akiendelea na ukaguzi wa kushtukiza wilayani Kakonko ili kuhakiki ubora na usalama wa bidhaa za chakula na vipodozi hususani muda wa mwisho wa matumizi.
Wakaguzi wa TBS wakiwa katika ukaguzi wa kawaida katika kiwanda cha kuzalisha maji ya kunywa wilayani Kibondo kijulikanacho kama " Malagarasi Mineral General Supply". TBS inawahimiza wazalishaji kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kuepuka usumbufu.
Mkaguzi wa TBS, Bw. Elisha Meshack akiwa kwenye ukaguzi wa bidhaa za vilainishi Wilayani Uvinza ambapo sampuli zilichukuliwa kwa ajili ya kupimwa katika maabara ili kujiridhisha kama zimekidhi ubora wa kiwango husika.

**********************************

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikishana na mkoa na Halmashauri husika, limeendelea na mpango wa ukaguzi wa kushtukiza sokoni kwa wasambazaji na wauzaji wa bidhaa za vilainishi, vipuli vya magari, vifaa ya ujenzi, chakula na vipodozi uliofanyika Kanda ya Magharibi Mkoani Kigoma katika wilaya za Kakonko, Kibondo, Buhigwe, Kasulu, Uvinza na Kigoma.

Ukaguzi huo umelenga kuhakiki iwapo bidhaa zinazouzwa soko ni kama zimekidhi ubora wa kiwango husika kulingana na ukaguzi uliofanyika katika maeneo ya uzalishaji na wakati zikiingizwa kutoka nje ya nchi, ili kuhakikisha wanapunguza tatizo la uwepo wa bidhaa hafifu sokoni aidha zinazoingizwa kupitia njia zisizo rasmi au kuzalishwa kwa kutozingatia matakwa ya kiwango husika.

Ukaguzi huo ulienda sambamba na utoaji elimu kwa wauzaji na wanunuaji juu ya uhifadhi sahihi wa bidhaa na umuhimu wa kuzingatia na kusoma taarifa sahihi na muhimu katika vifungashio.

TBS imefanya ukaguzi huu sambamba na usajili wa majengo ya chakula na vipodozi ili kuhakikisha majengo husika yanazingatia ubora na usalama wa bidhaa za chakula na vipodozi vinavyohifadhiwa au vinavyouzwa ndani ya majengo hayo.

Kaimu Mkuu wa Kanda ya Magharibi (TBS),Bw. Rodney Alananga ametoa wito kwa waingizaji na wauzaji wa bidhaa zilizo katika viwango vya lazima kuzingatia sheria na taratibu za uingizaji na uuzaji bidhaa kwa kuuza na kuingiza bidhaa ambazo ni bora na salama ili kukuza biashara na kuepuka kupoteza masoko na kero ya kukutwa na bidhaa hafifu ambayo itawalazimu kuziteketeza kwa gharama zao.

Pia aliwashauri wasisite kuwasiliana na ofisi ya TBS mara kwa mara pale wanapohitaji msaada wa kitaalamu.

Kwa upande wake Afisa Usalama wa Chakula (TBS ), Bw. Elisha Meshack alisema ukaguzi huo ni iendelevu kwani ni moja ya majukumu ya Shirika na utahusisha bidhaa mbalimbali katika sekta zote kasoro dawa na unaendelea pia katika wilaya za Mpanda, Tanganyika, Mpimbwe, Sumbawanga, Kalambo na Nkasi kwa upande wa Kanda ya Magharibi.

"Huu ni mwendelezo tu wa shughuli zetu za kila siku, kwani Shirika linahakikisha ukaguzi kama huu unafanyika katika kila wilaya nchi nzima ili kuhakikisha tatizo la bidhaa hafifu linapungua kwa kiasi kikubwa kama sio kwisha kabisa " alisema.

Afisa udhibiti ubora (TBS), Bw. Emmanuel Mushi aliwasisitiza wafanyabiashara wa maduka ya chakula na vipodozi ambao wamefanyiwa ukaguzi na kupewa gharama za malipo na bado hawajalipia gharama za usajili kulipia mara moja ili wapate kibali cha kuuza bidhaa husika katika majengo hayo ili kuepuka usumbufu na wale ambao hawajasajili majengo yao kusajili mara moja.

Meneja wa kiwanda cha kuzalisha maji wilayani Kibondo kijulikanacho kama "Malagarasi Mineral General Supply",Bw. Samir Adam ameipongeza TBS kwa kusogeza huduma karibu na amekuwa akipata ushirikiano wa kutosha kutoka ofisi ya kanda ya magharibi- Kigoma.

" Hapo mwanzo tulipoanza tulikuwa na changamoto ya kupata cheti na kutembelewa kwa wakati ila kwa sasa nashukuru ofisi ya TBS kanda ya magharibi iko jirani na inanipa ushirikiano mkubwa sana" alisema.

Pamoja na ukaguzi huo TBS inatumia fursa hiyo ya kukutana na mfanyabiashara mmoja mmoja kuelezea majukumu ya Shirika ikiwa ni pamoja na yale yaliyokua yakifanywa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa ( TFDA).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments