WAZIRI SIMBACHAWENE ATOA SIKU 30 KWA JESHI LA MAGEREZA KUWAHAMISHIA MAHABUSU GEREZA LA KARATU


Na Felix Mwagara, MOHA, Karatu.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene ametoa siku 30 kwa Jeshi la Magereza kuhakikisha Gereza jipya la Mahabusu Karatu linakamilika na kuanza kuhifadhi Mahabusu.

Amesema Mahabusu wa Wilaya ya Karatu waliohifadhiwa katika Gereza Kuu la Kisongo jijini Arusha wahamishiwe katika Gereza hilo ambalo ujenzi wake upo katika hatua ya mwisho kukamilika.

Akizungumza baada ya kukagua majengo ya Gereza hilo lililopo Mjini Karatu, leo, Waziri Simbachawene amesema muda wa mwezi mmoja unatosha kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo (CGP) kuhakikisha Gereza hilo linakamilika na kuanza kutoa huduma.

“Ifikapo tarehe 12 ya mwezi wa nne nataka mahabusu wawe wameanza kuletwa hapa badala ya kupelekwa katika Gereza la Kisongo, Arusha ambapo ni mbali sana, na gharama inakuwa kubwa, unaweza usione, lakini gharama yake inakuwa kubwa sana,” alisema Simbachawene.

Alisema Gereza hilo tayari lina mabweni mawili ya mahabusu pamoja na nyumba za askari, kwa muda ambao ametoa mwezi mmoja Jeshi hilo litaweza kukamilisha ujenzi wa Gereza na nyumba hizo kutokana na uwezo mkubwa alionao Mkuu wa Jeshi hilo katika kukamilisha kazi zake kwa uharaka.

Aidha, Waziri Simbachawene alifanya ziara katika Kituo cha Polisi Wilayani humo, ambapo alikikagua kituo hicho na kuzungumza na askari na maafisa wa Polisi wa Kituo hicho, ambapo amelitaka Jeshi hilo kutokujitenga na wananchi badala yake litengeneza urafiki na raia wema ili liweze kupata taarifa za mbalimbali uhalifu.

“Hakuna raia asiyejua polisi, kila mahali alipo raia na polisi wapo, nyie mnashughulika na mambo mengi sana katika jamii, mnasimamia ulinzi wa watu na mali zao, hivyo mnapaswa kushirikiana na raia katika kufichua wahalifu, kwa hiyo furaha, amani upendo katika jamii jeshi la Polisi linamchango mkubwa sana,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa Askari wanapaswa kushirikiana na raia ili kupata taarifa za Mkoa wa Arusha kwa kutoa huduma nzuri kwa wananchi ili kuleta imani kubwa kwa wananchi kwa kutenda haki kwa watu wote bila kujali kipato wala nafasi yake.

Pia Waziri Simbachawene, alikikagua kituo cha Polisi Kinachohusika na maswala ya utalii kilichopo wilayani humo ambapo amewataka Polisi hao kuboresha zaidi huduma katika vituo hivyo vya utalii kwa kuwahudumia watalii kwa haki pamoja na kuwa na lugha nzuri kwa wageni hao na pia kuwakamata madereva wanaoendesha magari ya watalii ambao watakuwa wanavunja sheria za usalama barabarani kwa kunywa pombe.

Alisema Watalii wakihudumiwa vizuri wanaenda kuhadithiana kuwa Tanzania ni wakarimu na huduma zao ni bora hivyo watalii wanaongozeka na Serikali inapata mapato wanapoingia Nchini.

“Katika kuwasimamia vizuri watalii wanaingia nchini kwanza mnapaswa kuangalia usalama wa magari wanayoyatumia, pili usalama wa magari na safari yenyewe, lazima uangalie kiwango cha madereva, kuna madereva wengine wanalewa, kuendesha watalii ile ni kazi inayohitaji umakini, wao watalii wamekuja kupumzika wanalewa wanafanya wanachotaka, wawe huru, lakini dereva hapaswi kulewa, wakamateni madereva hao watakaovunja sheria,” alisema Simbachawene.

Pia amewataka askari hususani wanao kuwa katika vituo hivyo vya utalii kuwa kioo kwa wageni wanaoingia nchini na wanaofika katika vituo vya utalii kupata msaada ili waitangaze Nchi vizuri kwa wageni hao wanaotoka mataifa mbalimbali duniani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments