WANANCHI WATAKIWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUPIMA AFYA KUBAINI MAPEMA DALILI ZA UGONJWA WA FIGO

 

Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dr. Luzila John akizungumza na mwandishi wa Malunde 1 blog ofisini kwake.

                          Na Josephine Charles - Malunde1 blog

Wito umetolewa kwa wananchi Mkoani Shinyanga kuwa na utamaduni wa kupima afya ili kubaini kama wana dalili za magonjwa yanayochangia ugonjwa wa figo.

 Wito huo umetolewa na Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dr. Luzila John wakati akizungumza na Malunde 1 blog ofisini kwake leo Machi 11 2021,Ikiwa Leo ni maadhimisho ya siku ya Figo Duniani.

Dk. Luzila ambaye ni Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani amesisitiza Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga  kupima Afya ili kubaini kama  wana dalili  za magonjwa yanayochangia kuwepo kwa maradhi ya Figo ikiwemo  Kisukari,Presha,Tezi Dume na HIV/UKIMWI ili kudhibiti Ugonjwa huo kabla haujasababisha madhara mwilini.

Amefafanua zaidi kuwa Watu wazima kuanzia umri wa miaka 40,wanatakiwa kujiwekea utaratibu wa kupima afya mara kwa mara, ili kuweza kujikinga na magonjwa ya figo.

 Katika hatua nyingine, Dk. Luzila ametahadharisha wananchi dhidi ya matumizi holela na makubwa ya dawa hususani za kienyeji bila kiwango maalum na ushauri wa kitaalam kwani hupelekea mwili kuwa na sumu nyingi na kuathiri Figo.

Aidha Kinga ya Ugonjwa sugu wa figo ni kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, kula lishe bora na kamili, kunywa maji angalau lita 2.5 kwa siku, usafi wa mwili, kutokuvuta sigara au kunywa pombe kupita kiasi pamoja na kudhibiti shinikizo la juu la damu, kisukari na maambukizi ya mara kwa mara ya mfumo wa mkojo.

Kila Alhamisi ya wiki ya pili ya mwezi Machi Dunia huadhimisha siku ya figo duniani,ambayo ilianza kuadhimishwa rasmi Mwaka 2006 katika nchi 66 na baadae kuenea katika nchi zote duniani, lakini Nchini Tanzania siku hii ilianza kuadhimishwa Mwaka 2011.

Lengo la kuadhimisha siku hii ni kufanya kampeni ya kidunia inayolenga kuongeza ufahamu kwa watu juu ya umuhimu wa figo na kuwahamasisha kuchukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya maradhi ya figo  na matatizo mengine ya kiafya yanayohusiana na figo.

Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “ ISHI SALAMA NA UGONJWA WA FIGO”

Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments