Picha : SAMIA SULUHU HASSAN AAPISHWA KUWA RAIS WA TANZANIA...IJUE HISTORIA YAKE HAPA


Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Machi 19, 2021 katika Ikuru ya Magogoni Mkoa wa Dar es Salaam. Ameapishwa leo baada ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kufariki Dunia Machi 17, 2021.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ameapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania na Jaji Ibrahim Juma katika Ikulu ya Jijini Dar es Salaam.
Mama Samia alikuwa Makamu wa Rais wa kwanza Mwanamke Tanzania na wa pili kwa Afrika Mashariki. Anakuwa Rais wa tatu mwanamke Afrika waliopitia mchakato wa kidemokrasia na wa kwanza kwa Afrika Mashariki.

Hafla ya kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan imefanyika Ikulu jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na viongozi na wageni mbalimbali.

Miongoni mwa viongozi hao ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa awamu ya awamu ya Nne Jakaya Kikwete na Aman Abeid Karume ambaye ni Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla hiyo.

Mwaka 2015, Rais Dkt.  John Pombe Magufuli alimchagua Samia Suluhu Hassan kuwa Mgombea Mwenza katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 na baada ya uchaguzi huo aliapishwa kushika Wadhifa wa Makamu wa Rais.

Historia hiyo ikajirudia tena Oktoba mwaka 2020 baada ya wawili hao kushinda uchaguzi Mkuu na kushika nafasi hiyo kwa muhula wa pili.

Akiwa na uzoefu wa kuwa Makamu wa Rais kwa zaidi ya miaka mitano sasa, Samia Suluhu Hassan ameapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akirithi nafasi ya Dk John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 kwa maradhi ya moyo katika hospitali ya Mzena jijini Dar es salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Samia ameapishwa na kuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano. Yaani mpaka mwaka 2025.

Ili kutekeleza majukumu yake mapya, kwa kushauriana na Chama cha Mapinduzi (CCM), atapendekeza jina la Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia 50.
Kwa sasa, Samia ndiye mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais na kuwa Rais nchini Tanzania. 

Atakuwa Rais wa pili wa Tanzania kutokea Zanzibar baada ya Ali Hassan Mwinyi aliyeiongoza kuanzia mwaka 1985 mpaka 1995.

Samia alizaliwa Januari 27 mwaka 1960 visiwani Zanzibar, anakuwa Rais wa kwanza Tanzania kuongoza Serikali baada ya mtangulizi wake kufariki akiwa madarakani.

Samia alisoma shule kadhaa za msingi kabla hajahitimu Mahonda iliyopo Unguja mwaka 1972 kisha akajiunga na Sekondari Ngambo na Lumumba hadi mwaka 1975. 

Mwaka 1977 Samia alijiunga na Taasisi ya Fedha na Utawala Zanzibar (ZIFA) alikotunukiwa cheti cha takwimu na kuajiriwa na Wizara ya Mipango na Maendeleo.

Baadaye alijiendeleza katika Taasisi ya Maendeleo na Utawala Mzumbe (IDM) ambayo sasa ni chuo kikuu kwa stashahada ya utawala.

Mwaka 1978 Samia aliolewa na Hafidh Ameir ambaye wakati huo alikuwa ofisa kilimo na mwaka 1989 alijiunga na Chuo cha Taifa cha Usimamizi na Utawala wa Umma cha nchini Pakstan kwa masomo ya utawala na mwaka 1991, alienda kusomea utawala kwa viongozi katika Chuo cha Hyaerabad nchini India.

Mwaka 1992, Samia aliajiriwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kisha akaenda Chuo Kikuu Manchester, Uingereza kwa masomo ya stashahada ya juu ya uchumi.

Samia pia ana shahada ya umahiri katika maendeleo ya uchumi aliyoisoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire cha Marekani.

Mwaka 2000 Chama cha Mapinduzi (CCM) kilimteua kuwa mwakilishi kupitia Viti Maalumu na akiwa kwenye Baraza la Wawakilishi aliteuliwa na Rais Amani Karume kuwa waziri.

Mwaka 2005 aliteuliwa tena hadi mwaka 2010 alipogombea ubunge katika Jimbo la Makunduchi alikoshinda kwa asilimia 80. Baada ya uchaguzi huo aliteuliwa kuwa Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais kushughulikia Muungano.

Mwaka 2014, Samia alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba lililoandaa Rasimu ya Katiba Mpya.
Jumapili ya Julai 12 mwaka 2015, Dk John Magufuli alipopitishwa kuwa mgombea wa urais wa CCM, Samia alikuwa mgombea mwenza.

Katika kinyang’anyiro cha ndani ya chama kilichoongozwa na Rais Jakaya Kikwete aliyekuwa mwenyekiti aliyemuelezea Dk Magufuli kama kiongozi mchapakazi, makini na asiyependa uvivu, kilimaliza makundi yaliyokuwapo kabla.

Kwenye kinyang’anyiro hicho, Dk Magufuli alipata kura 2,104 sawa na asilimia 87.08 hivyo kukabidhiwa bendera ya njano na kijani kukiwakilisha chama hicho na baada ya kunadi sera vilivyo, CCM ilishinda, Samia akaapishwa kuwa Makamu wa Rais.

Kutokana na kifo cha Dk Magufuli, Samia sasa anakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi kilichobakia mpaka mwaka 2025 utakapofanyika uchaguzi mkuu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments