WANNE WAKAMATWA KUZUSHA VIFO VYA CORONA TANZANIA, RPC ASEMA 'WANATIA HOFU'



Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia watu wanne kwa tuhuma ya kutumia mitandao ya kijamii kueneza uvumi wa vifo vya watu wakidai wamekufa kwa Corona na kutia hofu wananchi.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumatatu Februari 22,2021 ,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ACP Wankyo Nyigesa amewataja watuhumiwa hao kuwa  ni Frank  Almatia Nyange (47), Moses Goodluck Mgao (34) Mohamedi Lutambi (47) na Bumija Moses Senkondo (55) ambao walikamatwa Februari 18,2021 na Februari 19,2021.

“Watuhumiwa hawa wanne tuliowakamata na wengine ambao tunaendelea kuwatafuta wanasambaza taarifa za uvumi za vifo vya Watu wakidai wamekufa kwa Corona na pia wanapendekeza majina ya Viongozi wa Serikali ambao walitamani wafe haraka kwa Corona”,amesema Kamanda Nyigesa

Amesema watuhumiwa hawa wanne Frank Nyange na wenzake pamoja na wengine ambao wanatafutwa licha ya kueneza uvumi wa vifo vya watu wakidai wamekufa kwa Corona  pia wanatia hofu mitandaoni kwa kudai Watanzania walio wengi watakufa kwa sababu serikali haichukui tahadhari dhidi ya wananchi wake.

“Polisi Mkoani Pwani tunatoa rai kwa Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona kwa kufuata maelekezo ya Wataalamu wa Afya na kujiepusha na matumizi mabaya ya Mitandao ikiwemo kutoa taarifa za uvumi kuhusu vifo vya watu ambazo zinatia hofu wananchi wengi, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaofanya hivyo”,ameongeza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments