SHANGWE ZATAWALA SIMBA SC IKIICHAPA AL AHLY 1 -0


Shangwe, kuzomea, ngoma, vuvuzela na makofi, zimetawala ndani na nje ya Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam nchini Tanzania  baada ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Al Ahly ya Misri kumalizika wenyeji Simba wakiibuka na ushindi wa bao 1-0.

Bao la Simba lilifungwa kipindi cha kwanza na nyota wao machachari Luis Miquissone katika dakika ya 30 kwa shuti kali baada ya kuwahadaa mabeki wa Al Ahly na kufanya kipindi cha kwanza kumalizika wakiongoza.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko kwa kumtoa Hassan Dilunga na nafasi yake kuchukuliwa na Rally Bwalya ambaye aliingia kucheza nafasi ya kiungo na kuonyesha utulivu katika eneo hilo.

Pia katika kipindi cha pili timu zote mbili ziliendelea na mchezo wa kucheza kwa tahadhari na kushambulia kwa kusitukiza huku kwa Simba ingizo la Bwalya likionekana kuwa na changamoto kwa Ahly.

Winga wa Simba Luis Miqquissone alionekana kuwapa wakati mgumu walinzi wa Ahly kila alipokuwa na mpira jambo lililowafanya kumchezea madhambi mara kwa mara hususani kipindi cha pili.

Simba kwenye kipindi cha pili walionekana kucheza bila presha kubwa, huku umakini ukiongezeka katika ukabaji ambapo safu ya ulinzi iliyoongozwa na Pascal Wawa na Joash Onyango ilionekana kuwa na maelewano thabiti.

Zikiwa zimebaki dakika tano katika mechi hiyo kumalizika Simba walifanya mabadiliko mawili kwa kuwatoa Chris Mugalu na Luis Miquissone na nafasi zao zilichukuliwa na Meddie Kagere na Fransic Kahata. Pia dakika ya 90 walimtoa Clatous Chama na nafasi yake kuchukuliwa na Kennedy Juma mabadiliko ambayo yalilenga kulinda bao lao.

Kwa ushindi huo Simba inapanda kileleni mwa kundi A wakiwa na alama 6, AS Vita (3), Al Ahly (3) na Al Merrikh (0).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments