TANROADS YALIA NA TRAFIKI UHARIBIFU WA BARABARA, TEMESA YALALAMIKIA MADENI...TARURA, TANESCO WAANIKA MIPANGO



Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila (katikati) akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko na Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Dorice Dario.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila akizungumza wakati akiahirisha kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo leo katika ukumbi wa manispaa ya Shinyanga
***
Na Damian Masyenene, Shinyanga
KIKAO cha siku mbili cha Baraza la Madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga leo kimehitimishwa kwa kupokea taarifa za utendaji za taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Tanroads, Temesa, Tarura, Tanesco na Ruwasa pamoja na kupokea taarifa za utekelezaji wa kamati mbalimbali kwa robo ya pili 2020.

Akiwasilisha taarifa ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Shinyanga, Mhandisi wa Matengenezo, Emmanuel Maroa ameeleza kuwa askari wa jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani (Trafiki) wamekuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa miundombinu ya barabara kwa kusimamisha gari bila utaratibu na kupelekea vipande vya barabara kuliwa.

"Mbali na wizi wa taa za barabarani lakini pia tunaomba jeshi la polisi litusaidie kwa sababu maeneo yote ambayo trafiki wanasimama barabara imeendelea kuharibika, magari yanasimama poembeni (shoulder zinaliwa)… tunaomba jeshi la polisi watusaidie kutekeleza yale ambayo tuliwaomba ili barabara zetu ziwe salama. 

"Tuliwaomba tuwatengenezee maeneo maalum ili magari wanayoyasimamisha yaweze kusimama na yasiharibu barabara zetu. Pia tatizo lingine ni wananchi kulima maeneo ya madaraja na uchafuzi wa mazingira na miundombinu ya barabara," ameeleza.

Mhandisi Maroa amesisitiza kuwa katika mwaka huu wa fedha Tanroads wana mradi wa kuzikarabati taa zote za mjini na tayari mkandarasi ameanza kazi, huku akiomba maeneo ambayo taa hazifanyi kazi wataarifiwe ili kuzirekebisha.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Wilaya ya Shinyanga, Mhandisi Salvatory Yambi, akiwasilisha taarifa ya wakala hiyo ambayo ilipata wachangiaji wengi katika kikao hicho, ameeleza kuwa katika bajeti ya mwaka huu wamepanga kukabarabati barabara zenye urefu wa Km 771.74 ambapo wametengewa bajeti ya Sh Bilioni 1.47  kwa ajili ya kuboresha Km 102, kujenga makaravati 56 na kutengeneza Km 4.1 za mitaro.

Amebainisha kuwa katika bajeti ya mwaka huu wamekumbwa na changamoto ya kuchelewa kwa manunuzi, ambapo mpaka sasa mchakato wa manunuzi haujakamilika na hadi sasa miradi hiyo yote haijatekelezwa, huku akiahidi kuwa  changamoto hizo zitatuliwa.

"Tumelenga kwenda kutatua changamoto na mkakati wa kwanza ni kutatua maeneo korofi na yaliyoharibika, kwahiyo sehemu kubwa ya changamoto zitatatulika, tutasimamia kwa umakini mipango hii ya bajeti yetu ya Sh Bilioni 1.477," amesema.

Hata hivyo, katika kutatua changamoto zilizopo za maji kutuama wakati wa mafuriko, Mhandisi Yambi ameshauri halmashauri kutenga fedha zitakazosaidia kutatua changamoto za barabara na siyo kutengemea fungu la Tarura, elimu itolewe kwa wananchi juu ya uharibifu wa miundombinu ikiwemo kukemea utupaji taka hovyo kwenye mitaro, kuweka alama za makatazo kwenye hifadhi za barabara na kuanzisha njia maalum za kupitisha mifugo ili kuepuka uharibifu.

"Kitangiri na maeneo mengine watu wamejenga kwenye mikondo ya maji, tusitoe vibali kwenye maeneo ambayo kuna mikondo inayopitisha maeneo ya maji, inatuwia vigumu kutafuta njia za kupitisha maji ya mitaro," amesisitiza.

Wakichangia na kuuliza maswali juu ya taarifa ya Takukuru, Diwani wa Kata ya Ndala, John Koliba na na Ezekiel Sabo wa kata ya Ibinzamata, wameiomba Tarura kuona umuhimu wa kutenga bajeti ili kujenga daraja la dharura la miti kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanaotoka Ndala kwenda kusoma shule maalum ya wanafunzi jumuishi Buhangija wakiwemo wenye ulemavu mbalimbali, huku Diwani wa Kata ya Kitangiri, Mariam Nyangaka akiomba mkandarasi kupeleka greda kwa ajili ya kuondoa udongo uliosababishwa na mafuriko ya mvua iliyonyesha wiki iliyopita.

Akiwasilisha taarifa ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Kaimu Meneja Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Antony Tarimo
amesema kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 wameomba Sh Bilioni 2.42 na kupendekeza miradi 20 ya kuongeza miundombinu, kuboresha msongo wa umeme na kupanua huduma, huku wakiendelea kusambaza huduma ya umeme katika maeneo ya pembezoni kwani manispaa hiyo inavyo vijiji 7 ambavyo havina umeme.
 
Akifafanua hoja ya umeme wa REA, Mhandisi Tarimo amesema kuwa katika utekelezaji wa bajeti yao ya mwaka huu, hakuna vijiji ndani ya manispaa hiyo ambavyo vitapata umeme kupitia mradi wa REA, bali vitapata umeme kupitia utaratibu wa kawaida wa Tanesco.

"Tanesco tunapeleka mapendekezo, lakini kwa sasa tuna mradi wa PER URBAN unahusu maeneo ya pembezoni mwa mji….badala ya kung’ang'ania vijiji kupata umeme kupitia umeme wa REA ni vyema tukawaelekeza wananchi kupata umeme kupitia njia hii kwa sababu gharama ni zile zile (27,000) na unafadhiliwa na Serikali, umeanza katika baadhi ya mikoa, hivi punde mradi utaanza katika mikoa tuliyoomba ikiwemo sisi," amesema.

Kwa upande wao, Wakala wa Umeme (Temesa), wakiwasilisha taarifa yao kupitia kwa Daniel Ojwando, amesema kuwa wanashindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi kutokana na malimbikizo ya madeni wanayozidai taasisi za serikali, huku akiweka wazi kuwa wao siyo chanzo cha magari kukaa muda mrefu bila matengenezo bali halmashauri ndizo hazitoi mapema vibali vya matengenezo.

"Sisi hatuongezi bei, bali tunakagua matatizo yote yanayoisibu gari na kukushauri, lakini mtaani anaangalia tu tatizo ulilomwambia wakati gari inaweza kuwa na shida nyingi. Kwahiyo magari ambayo hayapiti Temesa yana matatizo mengi kwa sababu hayakaguliwi vizuri," amebainisha.

Akichangia katika taarifa ya Temesa, Diwani wa Kata ya Kizumbi, Ruben Kitinya, amesema kwamba madiwani na wasimamizi wa halmashauri hawaridhishwi na huduma zitolewazo na Temesa kwa vifaa vya halmashauri mfano greda linakaa muda mrefu wakati wananchi wanapata tabu uchafu unajaa dampo.

Baada ya uwaislishaji wa taarifa hizo, kikao hicho kilipokea taarifa za utekelezaji wa kamati za fedha na utawala, uchumi, elimu na afya na ile ya mipangomiji na mazingira katika kipindi cha robo ya pili mwaka 2020.

Akihairisha kikao hicho, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila amezitaka taasisi za serikali kufanya kazi kwa kushirikiana na kuwasiliana ili kuondoa changamoto zilizopo na kuitaka Tarura kuondoa tatizo la mitaro kujaa uchafu na michanga, huku akiiomba Tanroads kuufanyia akzi haraka ujenzi wa uwanja wa ndege kwani imekuwa kero na subira ya muda mrefu, ambapo amemuomba katibu wa Mbunge kulifikisha suala hilo kwa mbunge ili alipazie sauti bungeni na kuzikumbusha mamlaka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post