WAHANDISI MAJENGO WAOMBWA KUSAIDIA UJENZI WA VYOO SHULENI


Hiki ni choo cha muda kwa ajili ya wavulana wa shuleni Endesh
Maandalizi ya kujenga vyoo vya kudumu yakiwa yanaendelea shuleni Endesh

Na Abby Nkungu, Singida
WATAALAMU wa ujenzi wa majengo katika Halmashauri ya wilaya ya Singida wameshauriwa kutumia vyema taaluma zao kuwasaidia wazazi katika ujenzi wa vyoo bora na imara shuleni ili viweze kudumu kwa muda mrefu.

Hatua hiyo imedaiwa kuwa itaweza kuondoa kero ya kubomoka na kutitia kirahisi vyoo vya shule kila mara mvua zinapoanza kunyesha hali inayoleta adha kubwa kwa wanafunzi wanapokosa huduma hiyo muhimu

Rai hiyo ilitolewa na baadhi ya wanakijiji waishio jirani na shule ya msingi ya Endesh iliyopo mpakani mwa wilaya za Singida na Manyara, takriban kilometa 60 Kaskazini mwa mji wa Singida wakati timu ya Wanahabari ilipotembelea shule hiyo.

Wanahabari hao walilazimika kwenda kijiji cha Endesh kutokana na taarifa zilizotolewa kwenye Mkutano wa Wadau wa elimu uliofanyika Ilongero, Singida kwamba shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 570 haikuwa na vyoo.

Mkutano huo ulikuwa umeandaliwa na Shirika la Action Aid ambalo linatekeleza Mradi wa 'Kuvunja vikwazo, Haki kodi na Utoaji huduma kwa usawa wa kijinsia' katika shule 10 za halmashauri ya wilaya ya Chamwino, Dodoma na 10 halmashauri ya wilaya ya Singida mkoani Singida; Endesh ikiwemo.

"Ni kweli shule yangu haina vyoo vya kudumu isipokuwa tumejenga vya muda tu; kimoja chenye matundu matatu kwa ajili ya wavulana na kingine chenye matundu manne kwa ajili ya wasichana hali ambayo si njema kiafya", alieleza Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Elibariki Halai huku akiongeza;

Uwiano unaopendekezwa ni tundu moja kwa wavulana 25 na tundu moja kwa wasichana 20. Vyoo vyetu vya kudumu vilibomoka na kutitia mara msimu wa mvua ulipoanza. Hii inatokana na ujuzi duni wa mafundi wetu huku kijijini. Tunajiandaa kujenga vyoo bora na imara mara mvua zitakapokatika".

Wakati baadhi ya wanafunzi walithibitisha kuwa huwa wanakimbilia kwenye pori linalozunguka shule hiyo ili kujisaidia pale vyoo vinapobomoka, wengine walisema huamua kuacha kwenda shule kwa muda ili kukwepa adha ya kukosa mahali sahihi pa kujisaidia.

"Tunapoenda kujisaidia huko porini, tunajitoa mhanga kwani huko kuna nyoka na wanyama wengine wakali" ,alisema Jennipher George, mwanafunzi wa shule hiyo huku Mary Joseph akidokeza kuwa kukosekana vyoo imara na vyenye heshima shuleni hapo pia huchangia kiwango cha utoro wa wanafunzi shuleni.

Wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule hiyo walisema sababu kuu ya vyoo kubomoka na kutitia mara kwa mara inatokana na uhaba wa maarifa ya kutosha juu ya fani ya ujenzi wa vyoo kwa mafundi wengi wa vijijini; hivyo kutoa mwito kwa Wahandisi majengo wa halmashauri hiyo kusimamia kwa karibu ujenzi wa vyoo vya shule.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Singida, Elia Digha alikiri kuwa uhaba wa matundu ya vyoo kwenye shule nyingi katika halmashauri hiyo ni jambo linalowaumiza vichwa viongozi.

Hata hivyo, alisema kuwa iwapo kila mzazi atajituma vya kutosha katika kushiriki kwenye ujenzi wa vyoo vya shule kama ambavyo wanashiriki kujenga vyoo vyao nyumbani, hakutakuwa na shida kubwa kwenye shule.

"Kimsingi shule ni mali ya kijiji; hivyo jukumu la kujenga vyoo kwa ajili ya wanafunzi ni la wanakijiji wenyewe; hivyo wasisubiri kila kitu kutoka Serikalini", alisema Digha.

Aidha, aliwataka Wataalamu wa ujenzi wa majengo kuhakikisha wanatembelea shule zote za halmashauri hiyo ili kujiridhisha iwapo ujenzi wa vyoo vya wanafunzi katika kila shule unazingatia misingi ya ujenzi wa vyoo bora na imara.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, halmashauri ya wilaya ya Singida ina jumla ya shule za msingi 97 na 28 za Sekondari zilizosajiliwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments