AWESO ATOA SIKU SABA MKANDARASI KULIPWA DENI LAKE


Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akipanda kwenye tanki la Mradi wa maji Lusilile, Manyoni kujiridhisha na viwango vya ujenzi wake.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akikabidhi Mkataba kwa Jumuiya ya Watumiaji maji kwa mmoja wa wakazi wa kijiji cha Kashangu Itigi wilayani Manyoni. Wanaoshuhudia makabidhiano hayo ni Mbunge wa Manyoni Magharibi, Yahya Massare ( mwenye miwani) na Mkuu wa wilaya hiyo, Rahabu Mwagisa( kulia).


Na Abby Nkungu,  Manyoni

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amemwagiza Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Singida kumlipa ndani ya siku saba Mkandarasi wa Kampuni ya CMG Construction takriban Sh milioni 700 anazodai kutokana na kujenga tanki la kuhifadhia na kusambaza maji Lusilile wilayani Manyoni lenye ujazo wa lita milioni mbili.

Waziri Aweso alilazimika kutoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Manyoni Mashariki, Dk Pius Chaya kudai kuwa wananchi wake zaidi ya 50,000 katika vijiji 11 vilivyopo eneo hilo hawajaanza kunufaika na huduma ya maji ya mradi huo kutokana na Mkandarasi huyo kutolipwa deni lake.

"Lengo la mradi huu lilikuwa kupeleka maji kwenye Kituo cha Afya Kintinku na vijiji vilivyopo eneo hili lakini usambazaji wa maji unasuasua sana japo tanki lipo tayari." alisema Mbunge huyo na kuongeza;

Kituo hiki cha afya kinahudumia wananchi wa tarafa mbili; hivyo ni matamanio yangu huduma hii ya maji ifikishwe hapo mapema ili huduma nyingine za kiafya pia ziweze kufanyika ipasavyo".

Kutokana na hoja hiyo, Waziri Aweso alimuuliza Meneja RUWASA mkoa, Mhandisi Lucas Saidi iwapo ni kweli Mkandarasi huyo anaidai Serikali naye akathibitisha kuwa anadai takriban Sh milioni 700.

"Ndio maana mradi huu unasuasua. Hakikisha ndani ya siku saba Mkandarasi huyu awe amelipwa. Katoe Sh milioni 700 kwenye akaunti yenu umpe ili amalizie kazi wananchi waanze kupata huduma ya maji" aliagiza Waziri Aweso.

Akiwa kijiji cha Kashangu, Itigi Jimbo la Manyoni Magharibi, kwenye ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani Singida kukagua miradi mbalimbali ya maji, Waziri Aweso alielezwa kuwa jumla ya Sh milioni 150 ziliweza kuokolewa katika ujenzi wa mradi huo wa maji.

Meneja wa RUWASA wilaya ya Manyoni, Gabriel Ngongi alimweleza Waziri kuwa mradi huo ingawa ulitengewa jumla ya Sh milioni 350, lakini kwa kutumia wataalam wa ndani na mbinu nyingine mbadala, wameweza kutumia Sh milioni 200 tu; hivyo kuokoa Sh milioni 150.

Waziri Aweso aliipongeza hatua hiyo huku akiahidi kuwa Serikali haitakuwa kikwazo bali itatoa ushirikiano  wake wote kwa watumishi wanaojituma kama RUWASA Manyoni.

Aidha, alitoa mwito kwa wananchi wa eneo hilo na popote ilipo miradi ya aina hiyo Nchini kuitunza na kuilinda kwa nguvu zao zote kwa kuwa Serikali inatumia gharama kubwa katika kutekeleza miradi hiyo.  


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments