DC MACHA : HALMASHAURI ZIPIME MAENEO YA SHULE ZA MSINGI NA KUONYESHA RAMANI ZA VITU VYA KUJENGWA


Mkuu wa Wilaya ya Kahama Anamringi Macha akizungumza wakati akipokea madawati kutoka kwa Mdau wa maendeleo Idrisa Mohamed ili kusaidia wanafunzi wa Shule ya Msingi Kahama hafla hiyo iliyofanyika shuleni hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Anamringi Macha akizungumza wakati akipokea madawati kutoka kwa Mdau wa maendeleo Idrisa Mohamed ili kusaidia wanafunzi wa Shule ya Msingi Kahama hafla hiyo iliyofanyika shuleni hapo.

Na Neema Sawaka -Kahama
Serikali Wilayani Kahama mkoani Shinyanga imezitaka Halmashauri zote zilizopo katika wilaya hiyo kuhakikisha kuwa zinayapima maeneo yote ya shule za msingi zilizopo maeneo yao na kuonyesha ramani ya vitu vyote vinavyotakiwa kujengwa katika eneo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama Anamringi Macha alisema hayo wakati akikabidhi madawati 20 yaliyotolewa na mdau mmoja wa elimu Idrisa Mohamed kwa shule ya msingi Kahama kama mchango wake kwa shule hiyo aliyokuwa akisoma Elimu ya msingi.

Macha alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa maeneo hayo ya shule hasa zilizopo katika Manispaa yanapimwa na kuwekewa uzio na kuongeza kuwa zoezi hilo litaanza katika shule hiyo ya msingi ya Kahama na kuendelea katika shule zingine.

"Wananchi wa kawaida katika mji wa Kahama wamekuwa wakipimiwa viwanja vyao na Idara ya ardhi na inakuwaje sehemu zenye maeneo kama haya ya shule kuachwa kupimwa na kuongeza kuwa mikakati ya kupima itaanza kwa sasa ya kupima maeneo hayo",alisema.

‘Sisi kama Serikali tutaanza mikakati hiyo mara moja ya kupima maeneo mbalimbali ya shule hizo ili kuona kuwa maeneo yote ya shule za msingi yanapimwa na kutambuliwa kwa mipaka yake husika”, alisema Macha.

Alisema kuwa katika hatua nyingine changamoto inayoikumba shule hiyo ni ukosefu wa uzio huku baadhi ya wananchi wa maeneo hayo hutumia fursa hiyo katika kujisaidia katika vyoo vinavyotumiwa na wanafunzi wa shule hiyo ikiwa ni pamoja na watu waovu.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kahama Neema Elibariki alisema kuwa katika shule hiyo kulikuwa na upungufu wa madawati 22 na kuongeza kuwa baada ya mdau huyo kutoa msaada huyo yamebaki madawati mawili tu.

Alisema mbali na changamoto iliyokuwepo ya madawati pia kuna upungufu wa vyoo hali ambayo tunafanya jitihada za kukusanya fedha kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kufanikisha ujenzi huo polepole na tatizo hilo litakwisha.

Naye Mdau Idrissa Mohamed Yusuph alisema kuwa ni vema kwa wadau kuona umuhimu wa kusaidia katika shule walizokuwa wamesoma katika kipindi cha nyuma kwa kurudisha fadhira kwa kusaidia na kukumbuka maeneo walipotoka.

Mohamed ambaye ni mmiliki wa duka la Simu la Msomali Phone and Accessories la mjini Kahama alisema kuwa madawati hayo 20 aliyotoa yana thamani ya shilingi milioni 1.9 ili kupunguza tatizo la madawati katika shule hiyo aliyosoma na kuongeza kuwa shughuli zote za maendeleo haziwezi kufanywa na serikali tu pasipopo jamii kuwajibika.

Kaimu Afisa Elimu Misingi kutoka katika Manispaa ya Kahama Anna Kiya alisema kuwa wadau wamefanya kitu kizuri katika kukumbuka mahali ambapo walisoma katika kipindi cha nyuma na kuamua kutoa kidogo walicho nacho kusaidia wenzao.

Kiya aliwaomba wanafunzi waliosoma katika shule hiyo kuiga mfano wa Idrisa huku akiwataka wanafunzi kuhakikisha kuwa madawati hayo yanatunzwa na kudumu kwa miakam iliyopungua mitano.

Alisema kuwa shule hiyo ina wanafunzi 966 na walimu wakiwa 23 na kuongeza kuwa msaada huo ni mkubwa na kuongeza kuwa wanafunzi wa watu walikuwa wanakaa dawati moja kwa hiyo ni jambo la kushukuru kwa kupata msada huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments