IFAHAMU HISTORIA YA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD


Maalim Seif Sharif Hamad alizaliwa Oktoba 22, 1943 na alipitia Shule za Uondwe na Shule ya Wavulana ya Wete Kisiwani Pemba kati ya 1950 – 1957.

Sekondari alisomea katika shule ya King George VI Memorial mjini Zanzibar, na aliendelea na masomo ya cheti cha cha sekondari katika shule hiyo.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia 1972 -1975 na kuhitimu na shahada ya sayansi ya siasa, utawala wa umma na mahusiano ya kimataifa.

Amekuwa katika siasa za Zanzibar tangu miaka ya 1970, akiwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri wa Elimu kati ya 1977 – 1980, na mjumbe mwazilishi wa baraza la wawakilishi visiwani humo.

Baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania mwaka 1992, Hamad pamoja na wanachama wengine wa zamani wa CCM waliunda Chama cha Wananchi CUF.

Machi 2019, Maalim alijiunga na Chama cha ACT Wazalendo ambacho amekuwa nacho mpaka kifo kilipomkuta ambapo amehudumu kama Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Jina lake likarudi tena kwenye ulingo wa siasa kwa kasi sana. Shamrashamra,nderemo na vifijo vilisikika katika viunga vya Visiwani Zanzibar na Tanzania Bara.

Baada ya Maalim Seif Sharif Hamad kuachana na CUF alikohudumu kwa kipindi cha miaka 26, baada ya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam kumthibitisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho mnamo Machi 18 mwaka huu.

Maalim Seif ndiye Katibu mkuu wa muda mrefu wa chama cha siasa nchini Tanzania, ambapo tangu kuanzishwa chama hicho mwaka 1992 hakijawahi kuwa na katibu mwingine.

Maalim Seif alijiunga na chama kipya ACT-Wazalendo kinachoongozwa na mwanasiasa machachari Zitto Kabwe, ambaye pia alikuwa Mbunge pekee wa chama hicho akiwakilisha jimbo la Kigoma Mjini.

Kishindo cha Maalim Seif Sharif Hamad kujiunga ACT Wazalendo kiliibua Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania na kukiandikia barua chama hicho kijieleze na kutishia kukifuta kwa madai ya mbalimbali yaliyoanishwa kwenye barua yake.

Sakata la Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini na ACT-Wazalendo lilianzia kwenye maeneo matatu; Kwanza, Msajili alikituhumu na kukionya chama hicho kwa madai ya kutumia maneno ya dini (Takbir) katika siasa jambo ambalo linakatazwa.

Pili, Msajili alikituhumu kukiuka sheria ya vyama vya siasa kwa kutopeleka kwake hesabu zilizokaguliwa mwaka 2013/2014 kama sheria inavyotaka.

Tatu, Msajili alituhumu chama hicho kuhamasisha vurugu na uchochezi kwa kile kilichoitwa wanachama na mashabiki wa Maalim Seif kuchoma moto bendera na kadi za uanachama za chama cha Wananchi-CUF.

Aidha, Msajili alifafanua kuwa kitendo hicho kinavunja vifungu vya 9(1)(c) na 9(2)(a) vinavyokataza kuchanganya shughuli za vyama vya siasa na dini. Tuhuma hizo zilijibiwa na ACT Wazalendo ndani ya siku 14 kama kilivyoelekezwa na Ofisi ya Msajili.

Akiongea na wanahabari baada ya kutolewa kwa barua hiyo, Maalim Seif alisema kinacholengwa si chama cha ACT, bali yeye akidai kuwa amekuwa akichukuliwa kama tishio kwa watawala.

Kupaa na kutunguliwa ndani ya CCM
Uamuzi wa kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo unamaanisha kuwa Maalim Seif amejiunga na chama cha tatu tangu alipojitumbukiza kwenye siasa. Awali Maalim Seif alikuwa mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo mwaka 1988 alifukuzwa ndani ya CCM akiwa na wenzake, Shaban Mloo,Ali Haji Pandu,Khatib Hasan, Soud Yusuf Mgeni, Hamad Rashid na Ali Salim. Duru za kisiasa zinaonyesha kuwa akiwa CCM amewahi kuwa Mjumbe Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Waziri wa Elimu wa visiwa hivyo kati ya mwaka 1977-1980.

Maalim Seif alikuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la kati ya mwaka 1980-1989, pia Mbunge wa Jamhuri ya Tanzania mwaka 1977. Aidha, alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kati ya mwaka 1977 hadi 1987 pamoja na kuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango wa CCM.

Baadaye alikuwa waziri kiongozi wa Zanzibar kuanzia Februari 6, 1984 hadi Januari 22, 1988. Hata hivyo mwaka 1988 ulikuwa wa mwisho kwake kuwa kuwa mwanachama wa CCM, baada ya kufukuzwa kutokana na mgogoro wake na maofisa wa chama hicho.

Miongoni mwa rekodi ya kukumbukwa ni kwamba jina la Maalim Seif linaleta sura nyingine ya mgongano mkubwa wa maslahi ndani ya CCM Zanzibar, kati yake na aliyekuwa Rais wa visiwa hivyo Aboud Jumbe.

Duru za kisiasa zinamtaja kuwa Maalim Seif ndiye mwanasiasa aliyemdokeza Mwalimu Julius Nyerere kuhusu azima ya Rais Jumbe kuhoji muundo wa muungano. Rais Jumbe pia alichukua uamuzi wa kumfukuza kazi Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Jaji Damiani Lubuva na badala yake akataka kumwajiri mwanasheria kutoka Ghana.

Tangu kutunguliwa kwake CCM, Maalim Seif hajachuja kisiasa, ambapo alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliokuwa kwenye vuguvugu la KAMAHURU(Kamati ya Mwelekeo wa Vyama Huru), ambayo baadaye iliunda chama cha CUF.

Kwa kipindi cha miaka 26 Maalim Seif amepambana na utawala wa CCM bila kuchoka, na bila kurudi nyuma. Amesimama kidete na kuhakikisha masilahi ya wananchi wa Zanzibar yanalindwa. Matokeo ya jitihada zake katika siasa ni mengi, lakini kubwa zaidi ni kuundwa kwa nafasi ya makamu wawili wa rais wa Zanzibar.

Vilevile kuchochea mageuzi makubwa ndani ya Tanzania. Maalim amepambana na vigogo wakubwa kwenye chaguzi za kisiasa tangu mwaka 1995 (Salmin Amour), mwaka 2000 na 2005 (Amani Karume, mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar Abeid Karume), mwaka 2010 na 2015 (Dk. Ali Mohammed Shein).

Kinachoshangaza, Maalim Seif ni tofauti na wanasiasa mbalimbali waliohama CCM na kujiunga upinzani. CCM wenyewe walimfukuza Maalim Seif, lakini hajawahi kurudi nyuma wala kupungua makali kisiasa, tofauti na wenzake kama vile Augustine Mrema, Edward Lowassa,Frederick Sumaye na wanasiasa wengine.

Swali kubwa hapa ni kwamba, je harakati zote zinazofanywa dhidi ya Maalim Seif linaashiria kuwa ni ‘mtu hatari’ katika siasa za Tanzania?

Aghalabu akiwa Cuf wanachama wake wamekumbana na rungu la Jeshi la Polisi hususani wakati wa uongozi wa IGP Omar Mahita ambapo pande zote mbili zilituhumiana mambo mbalimbali yanayoashiria uvunifu wa amani. Wakati wafuasi wa Cuf alipojiita Ngangari, naye aliyekuwa IGP Mahita akasema yeye ni Ngunguri.

Hekaheka za CUF ya Maalim Seif na vyombo vya usalama imetuletea tafakuri hii. Ndiyo kusema Maalim Seif amepambana kwa namna yake katika siasa kiasi cha kuwatisha watawala ambao kila kukicha wamekuwa ‘wakimshughulikia’ kwa namna mbalimbali, ambapo sasa wanakitishia kufuta usajili wa chama kipya alichohamia, ACT Wazalendo.

Kupaa kwa ACT-Wazalendo
Je harakati hizi za kuondoka kwa Maalim Seif kutadhoofisha siasa za CUF visiwani Zanzibar? Hilo ndilo swali linalotakiwa kutafutiwa majibu kwa sasa, ambayo kwa haraka ni sawa na kusema ni kutunguliwa kwa chama cha CUF na kupaa kwa ACT-Wazalendo katika siasa za visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Mathalani, vyombo vya habari vimeripoti kuwa wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) jijini Tanga, kutoka Kata 27 na matawi 96, wamemfuata mwanasiasa huyo ikiwa ni saa chache baada ya kutoa tangazo la kuhamia ACT-Wazalendo.

Kimsingi madhara ya kuondoka Maalim Seif ndani ya chama cha CUF na kuhamia ACT-Wazalendo ni lazima yaonekane, bila kujali yawe ya muda mfupi au mrefu.

Ni lazima madhara yake yatakuwepo ikiwemo kudorora kwa ushawishi wa CUF katika siasa za Zanzibar, na kupoteza sehemu kubwa ya ushawishi wao waliokuwa nao tangu mwaka 1992 visiwani Pemba. Hekaheka zinazoendelea visiwani Zanzibar kwa sasa zimetoa dalili za wazi kuwa ACT-Wazalendo kinakwenda kushika hatamu katika siasa za Zanzibar.

Sehemu ya kwanza ambayo itakiathiri chama CUF ni majimbo ya uchaguzi yaliyoko visiwani Pemba. Tangu kurudishwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi nchini mwaka 1992, majimbo ya visiwani Pemba yameongozwa na wanasiasa kutoka upinzani hasa CUF.

Duru za kisiasa zinabainisha kuwa wananchi wa Pemba ‘hawataki’ kuongozwa na kuwa na wawakilishi kutoka chama cha CCM. Wananchi wao wanahitaji kitu tofauti cha kuwanganisha nacho si chama cha CCM.

Aidha, wananchi wa visiwa hivyo wanasifika kwa kuwa msimamo ya hali juu linapofika suala la siasa na masilahi yao, ikiwemo kuvithamani,kuvilinda na kuwapigania viongozi wao bila kuchoka au kujali kama wameshinda au la. Ushawishi wa chama cha ACT-Wazalendo utapanuka na kukua kwa kasi visiwani Pemba na Unguja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post