AKIPATA CHA MOTO BAADA YA KURITHI MKE WA JAMAA WALIYEMZUSHIA AMEFARIKI



Sokomoko ilizuka katika nyumba moja eneo la Aboloi Teso, nchini Kenya baada ya jamaa kurejea nyumbani na kumshambulia jirani yake aliyekuwa “amemrithi” mkewe. 

Duru zinaarifu kwamba jamaa alipandwa na hasira alipofika kwake na kupata jirani yake amepiga kambi katika boma lake.

Kulingana na Taifa Leo, baada ya jamaa kuoa miaka minne iliyopita alielekea jijini kutafuta kazi na akamuacha mkewe kijijini. 

Penyenye zinasema, jirani yake aliamua kumrithi mke wa jamaa baada ya tetesi kuibuka kuwa jamaa huyo huenda alikuwa ameaga dunia. 

Haijulikani haswa ni nani alianza kueneza uvumi huo.

Semasema zinaarifu kwamba hivi majuzi jamaa alifunga safari kutoka mjini bila kumjulisha yeyote na alipofika alimkuta njemba akiwa ametawala nyumbani mwake.

“Unafanya nini kwa nyumbani kwangu na mke wangu,” jamaa alimngurumia jirani yake. Jirani alishindwa apitie wapi ili ahepe kichapo kilichokuwa kimemkodolea macho.

 “Nilipata habari kuwa umemrithi mke wangu. Ulimrithi kama nani,” jamaa alimuuliza jirani yake.

 Habari ziliwafikia majirani kuhusu kisanga hicho nao wakatoka mbio kwenda nyumbani humo kuthibitisha ni kweli jamaa waliyedhani amefariki dunia alikuwa amerejea.

“Hauwezi kumrithi mke wangu na mimi mwenyewe ningali hai. Leo utajua mimi ni nani,” poo aliapa huku akirudi nyuma kuokota mpini wa jembe atwange jirani.

 Penyenye zinasema kuwa katika harakati ya jamaa akurudi nyumba kuokota mpini, jirani alipata mwanya wa kuhepa na akachomoka mbio kuingia mafichoni.

 “Hata ukitoroka uende wapi lazima nitakutafuta. Kwako ni hapa tu,” jamaa aliwaka huku majirani wakipasua kicheko. “Kazi ya huyu jamaa ni kunyemelea wanawake wa wenyewe. Leo amekipata. Na bado!” jirani mmoja alisikika akisema.

 Inasemekana jamaa hakukomea hapo kwani aliwatahadharisha waliokuwa wakieneza uvumi eti alifariku dunia. “Waliotangaza kuwa mimi nimekufa sasa aibikeni. 

Ninajua huyu jirani yangu ni mmoja wa wale wenye kueneza porojo hizo. Atanitambua. Sijamalizana nay eye,” jamaa aliapa huku akisema hakuwa na shida hata kidogo na mumewe licha ya kumkuta akila vya haramu na jirani.

 Chanzo - Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments