KUTANA NA NDEGE WA AJABU MWENYE JINSI MBILI...NUSU JIKE, NUSU DUME


Ndege ambaye ameonekana kuwa nusu-jike na nusu-dume amepigwa picha jimboni Pennsylvania na mfuatiliaji ndege baada ya kumsikia rafiki yake ambaye alimuona ndege huyo.

Ndege wa namna hii mwenye maumbile mchanganyiko ni nadra kuonekana.

Ndege aina ya cardinals dume ni wekundu lakini jike huwa ni rangi ya udongo iliyofifia, ikimaanisha kuwa spishi za ndege huyu pengine ni mchanganyiko wa jinsi mbili.

Mtaalamu wa masuala ya ndege Jamie Hill, 69, ameiambia BBC kuwa ilikuwa ni ''mara moja katika maisha, mara moja kati ya milioni''. Kukutana na ndege huyo.


Ndege wa kushangaza

Rafiki wa Bwana Hill alimwambia amemuona ''ndege asiye wa kawaida'' akifika katika malisho ya ndege katika kaunti ya Warren huko Pennsylvania.

Mara ya kwanza Bwana Hill alijiuliza ikiwa ndege huyo alikuwa na athari ya melanini kwenye manyoya yake, lakini hatakuwa nusu-jike, nusu-dume.

Lakini baada ya kuona picha kwenye simu, alishuku kuwa ndege huyo alikuwa na jinsia mbili, maana yake akiwa na ovari inayofanya kazi na korodani inayofanya kazi.

Alitembelea eneo ambalo ndege huyo alionekana.

Ndani ya saa moja aliweza kumpiga picha ndege huyo wa ajabu.

''Baada ya kupata picha, moyo wangu ulikuwa unadunda kwa saa tano mpaka nilipowasili nyumbani na kuzitengeneza picha ili kuona kile nilichonacho,'' alisema Bw.Hill.


Jamie hill amekuwa akichunguza kwa miaka 48

Ndege nusu-jike, nusu-dume ni nadra kupatikana, anaeleza profesa Brian Peer kutoka Chuo cha Illinois, ambaye amekuwa akifanya utafiti viumbe vya namna hiyo nchini Marekani.

Lakini, anaongeza kuwa hali hiyo inaweza isigundulike kwa baadhi ya spishi.
''Hali hii husababishwa na hitilafu wakati wa mgawanyo wa seli wakati wa kuumbwa kwake,'' alisema.

Ndege wa namna hii si mara ya kwanza kuonekana katika eneo hilo.

Mwaka 2019, wenza walimshuhudia ndege kama huyo, kwa mujibu wa jarida la National Geographic. Bwana Hill anashuku kuwa ndege ailiyemuona huenda akawa huyo huyo.

CHANZO - BBC SWAHILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post