Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, Bw Stanley Kafu (wa nne kushoto) akiwasilisha mfano wa hundi yenye thamani ya sh mil 10/- kwa Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Asma Mwinyi Foundation (AMF) Bi Asma A.H Mwinyi (wa tatu kulia) kwa ajili ya kuwezesha ununuzi wa vifaa vya ujenzi na ukarabati wa vyoo vya Shule ya Awali, Msingi na Sekondari ya Kandwi iliyoko Unguja, Zanzibar. Wanaoshuhudia ni pamoja na Meneja Mwandamizi wa benki ya Exim Zanzibar Bw Mwinyimkuu Ngalima (wa tatu kushoto), maofisa wa benki hiyo pamoja na wawakilishi wa shule hiyo.
NA MWANDISHI WETU
Benki ya Exim imetoa kiasi cha Sh milioni 10
kwa taasisi ya Asma Mwinyi Foundation (AMF) kwa ajili ya kuwezesha ununuzi wa
vifaa vya ujenzi na ukarabati wa vyoo vya Shule ya Awali, Msingi na Sekondari
ya Kandwi iliyoko Unguja, Zanzibar.
Hatua hiyo ni sehemu ya dhamira endelevu ya
benki hiyo katika kusaidia sekta za elimu na afya nchini.
Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki
ya Exim, Bw Stanley Kafu, aliwasilisha msaada huo kwa Bi Asma A.H Mwinyi ambaye
ni Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi AMF katika hafla ya
makabidhiano ambayo ilifanyika katika viwanja vya shule hiyo mapema hii leo
Zanzibar.
“Tumejitolea kuhudumia watu, biashara na jamii
kwa ujumla. Benki ya Exim na AMF kwa pamoja tuna dhamira inayofanana ya
kusaidia juhudi za kielimu na ustawi wa wanafunzi wetu na shule kote nchini.
Wanafunzi hutumia muda mwingi zaidi katika siku wakiwa shuleni hivyo ni muhimu
zaidi tukiweka jitihada katika kuboresha mazingira ya vyoo vyao,'' alisema.
"Tunafurahi kuwa sehemu ya mkakati huu
muhimu unaolenga kuinua mazingira ya elimu Zanzibar. Tunaona kwamba taasisi ya
AMF kuwa mshirika sahihi katika kufanikisha dhamira hiyo. Benki ya Exim
tumekuwa wadau wakubwa katika kusaidia sekta ya elimu katika jamii yetu, na
tunatarajia kupanua juhudi hizo hapa Zanzibar.’’ Aliongeza
Ikiwa ni taasisi isiyojiendesha kibiashara
yenye makao yake nchini, AMF imejikita zaidi katika kukuza programu ambazo
zinaboresha maendeleo ya jamii katika mazingira ya vijijini na mijini,
kushughulika haswa na wasichana na wanawake wenye mahitaji ya elimu, afya, na
mahitaji mengine ya msingi katika jamii zao.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwanzilishi
na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya AMF Bi Asma A.H Mwinyi aliishukuru benki
ya Exim huku akibainisha kuwa msaada huo utagusa maisha ya wanafunzi wengi kwa
miaka mingi ijayo.
"Wadau wetu muhimu na washirika kama Benki
ya Exim ndio nguzo muhimu kwa mafanikio yetu. Tunashukuru kwa msaada huu ambao utasaidia
katika kukarabati vyoo vya Shule ya awali, Msingi na Sekondari ya Kandwi,''
alibainisha.
Kulingana na taarifa ya wasemaji wa shule hizo,
Bw Kheir Juma Pandu na Juma Haji Ame walieleza kuwa, kukamilika kwa ujenzi na
ukarabati wa vyoo hivyo kutasaidia kuhudumia wanafunzi zaidi 700 waliopo katika
shule hiyo.
"Tunatumahi kuwa ukarabati huu utasaidia
watoto kuzingatia kwa zaidia masomo yao," walieleza.
Zaidi alitoa wito kwa taasisi zingine za
kifedha na wadau wanaopenda kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha
mazingira ya kujifunzia katika shule za umma nchini kujitokeza kwa wingi katika
jitihada hizo.