Magari yaliyopata ajali na kuua watu wanne
**
Watu wanne wamefariki dunia, akiwamo Afisa Ugavi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) mkoa wa Simiyu, Castory Mamboleo (35), kufuatia ajali iliyohusisha magari mawili wilayani Bariadi, mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu, ACP Richard Abwao, amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kusema kuwa ajali hiyo imetokea Februari 26, 2021, saa 1:30 jioni katika eneo la Dutwa wilayani Bariadi, ambapo mpaka sasa chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa.
Kamanda Abwao amewataja watu wengine waliopoteza maisha katika ajali hiyo ya barabarani kuwa ni Penina Naveta (38) ambaye ni Afisa Utumishi wa RUWASA mkoa wa Simiyu, Raphael Kichele (30) mfanyabiashara na Ntobi Mpalala ambaye ni mtoto mwenye umri wa miaka7, mwanafunzi na mkazi wa Dutwa.
Magari yaliyogongana na kusababisha vifo vya watu hao ni T 851 DKF Toyota Mark X na T 350 DUH, TATA BUS mali ya kampuni ya Ngalabushi, iliyokuwa ikiendeshwa na Paulin Abel (31) mkazi wa Lamadi, na kusema kuwa basi hilo lilikuwa likitokea Lamadi kuelekea Bariadi.