WAZIRI MKUU MAJALIWA: UBORA WA MIRADI ULINGANE NA THAMANI YA FEDHA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema miradi yote inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini lazima isimamiwe vizuri ili kuhakikisha inakuwa na viwango vinavyoendana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali.

“Maelekezo ya Serikali kwenye maeneo yote muhimu ya miradi isimamiwe kwa kina na hasa thamani ya fedha na viwango vya ujenzi wa miradi yenyewe. Tumeona Sekondari ya Tunduru, majengo ya halmashauri ya wilaya ya Mbinga, barabara ya Mbinga-Mbamba Bay na uwanja wa ndege utaalamu umetumika na thamani ya fedha ipo.”

Ametoa agizo hilo jana (Jumatano, Januari 6, 2021) alipozungumza na viongozi wa mkoa wa Ruvuma katika Uwanja wa Ndege wa Songea akiwa njiani kuelekea Dar es Salaam. Uwanja huo kwa sasa unakarabatiwa ili kuimarisha huduma za usafiri wa anga mkoani Ruvuma.

Amesema zaidi ya shilingi bilioni 37 zimetumika kuimarisha uwanja huo kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma. Ukarabati huo umehusisha njia ya kurukia ndege yenye uwezo wa kupokea abiria zaidi ya 150, jengo la abiria na maeneo ya maegesho yenye uwezo wa kuegesha ndege kubwa sita. Uwanja huo utakapokamilika utaruhusu ndege kutua usiku na mchana.

Waziri Mkuu amewataka viongozi hao waendelee kuwahamasisha wananchi kutumia fursa hiyo ya uwepo wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali katika kufanya biashara ili kukuza uchumi wao kwa kuwa wana miundombinu ya kutosha.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi hao wahakikishe wanasimamia matumizi ya miundombinu ya miradi mbalimbali iliyokamilika ili iweze kutumika vizuri zaidi na kwa muda mrefu.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments