WAZIRI MKUU ATOA SIKU MBILI SEKONDARI YA TUNDURU IPELEKEWE GARI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempa siku mbili Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoni Ruvuma, Gaspar Balyomi awe amepeleka gari katika shule ya Sekondari Tunduru kwa ajili ya kuwahudumia walimu na wanafunzi shuleni hapo.

Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Januari 2, 2021) wakati alipokagua ukarabati wa Shule ya Sekondari Tunduru. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya mbunge wa Tunduru Kusini, Daimu Mpakate kumueleza kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya usafiri.

“Mkurungezi Jumatatu lete gari moja hapa likiwa limeandikwa Shule ya Sekondari Tunduru lije kutoa huduma kwa watoto na walimu wetu. Hii shule inawanafunzi zaidi ya 600 na walimu 28 lazima iwe na usafiri ambao hata mtoto akiugua afikishwe hospitali.”

Kuhusu ukarabati uliofanyika shuleni hapo, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ametumia fursa hiyo kumpomgeza Mkuu wa Shule, Mwalimu Amini Limia pamoja na kamati ya ujenzi kwa kazi nzuri ya usimamizi waliyoifanya.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani ilianzisha mkakati wa kukarabati shule zote kongwe nchini ikiwemo ya Shule ya Sekondari ya Tunduru ambayo ukarabati wake umegharimu zaidi shilingi milioni 700. Mkoa wa Ruvuma umepewa jumla shilingi bilioni 3.7 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe za sekondari ikiwemo ya Tunduru.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi wazingatie sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa shuleni hapo ili waweze kuishi vizuri. “Someni hasa sasa hivi ni wakati wa likizo mpo hapa mnaendelea na masomo hatutarajii mpate daraja la nne wala sifuri. Kila mmoja ahakikishe anasoma na kupata daraja litakalomfikisha chuo kikuu.”

Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na ufualu wa wananfunzi wa shule hiyo katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo ambapo wanafunzi wote wa kidato cha sita walifaulu kwa zaidi ya asilimia 90. Amesema anatarajia katika matokeo ya mwaka huu watafaulu kwa asilimia 100.

Awali, Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Limia alisema walipokea zaidi ya shilingi  milioni 792 kutoka Serikali kupitia mpango wa EP4R kwa ajili ya ukarabati wa majengo 15 ambayo yalikuwa yanakabiliwa na uchakavu mkubwa kutokana na kujengwa miaka 38 iliyopita.

Alisema ukarabati huo pia ulihusisha ujenzi wa majengo mengine mawili ambayo ni matundu 12 ya vyoo kipya cha wanafunzi na kibanda cha mlinzi. “Majengo yaliyokarabatiwa ni jengo la utawala, bwalo na jiko, madarasa vyumba 16, mabweni sita, jingo la zahanati, jingo la duka na stoo, vyoo majengo manne pamoja na kukarabati mfumo wa maji taka nje ya majengo.”

Shule ya Sekondari Tunduru ni miongoni mwa shule kongwe nchini ambayo ilianzishwa mwaka 1982 na ni ya wavulana kwa kidato cha tano na sita katika michepuo ya PCM, PCB, PGM, CBG, HGL, HGK NA HKL na ina jumla ya wanafunzi 682 na walimu 28.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post