WALIMU WAKUU SHULE ZA MSINGI WATAKIWA KUSIMAMIA FEDHA ZINAZOTOLEWA NA SERIKALI


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amewataka walimu wakuu wa shule za msingi nchini kuhakikisha wanasimamia fedha zinazotolewa na Serikali  kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu  kwa kufuata sheria na taratibu katika matumizi.

Akifungua mkutano mkuu wa pili wa umoja wa walimu wakuu wa shule za msingi Tanzania Bara jana , Jijini Dodoma Mhandisi Nyamhanga amesema serikali inapeleka fedha  za ruzuku mashuleni kwa kila mwezi ili ziweze kununua vifaa vya kufundishia, kujifunzia hivyo ni jukumu la  walimu  kusimamia kwa umakini na kuhakikisha wanafunzi hao wanapata elimu bora.

Mhandisi Nyamhanga anafafanua kuwa Serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha elimu ya msingi hapa nchini inakuwa bora kwa kuboresha miundombinu ya elimu, hivyo ni wajibu wa Wakuu wa Shule za Msingi kuhakikisha fedha hizo zinasimamiwa kikamilifu.

“Serikali iko makini kuhakikisha suala la elimu linakuwa mbele zaidi kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya maboresho ya miundombinu katika ujenzi wa vyoo,nyumba za walimu na mabweni ni kazi yenu kuhakikisha fedha hizo zinasimamiwa ili ziweze kutumika katika miradi iliyokusudiwa ,”amefafanua Mhandisi Nyamhanga

Mhandisi Nyamhanga amesema Serikali imeweka mikakati ya kuimarisha elimu ya msingi na kusisitiza kuwa fedha za programu ya elimu bila malipo zitatumika kufidia malipo ya ada,posho kwa walimu wakuu pamoja na huduma nyingine za msingi.

Aidha, Nyamhanga ametumia fursa hiyo kuweka wazi kuwa Serikali inalaani vitendo vya udanganyifu wa mitihani na kuwataka walimu wakuu nchini kuendelea kudhibiti vitendo hivyo ili kuboresha elimu ya msingi.

“ Ni jambo la kusikitisha kuona katika ulimwengu huu bado walimu hamuwezi kudhibidi wizi wa mitihani,tunawakatisha tama wanafunzi wanaojituma,”amesema Mhandisi Nyamhanga.

Mhandisi Nyamhanga amesema vitendo vya udanganyifu wa mitihani bado ni tatizo ambalo lipo linatia doa  doa  kubwa kwani kwa kipindi cha mwaka jana pekee jumla ya wanafunzi 1065 walifutiwa matokeo ya mitihani kwa udanganyifu na kuwataka walimu hao wakuu kuangalia namna ya kudhibiti na kwamba hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa watakaovujisha .

Wakati huo, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais –TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Gerald Mweli ametoa rai kwa umoja huo kujituma katika kutoa elimu bora kwa jamii ili kuzalisha wataalamu watakaotosha nchini.

Naye Rehema Ramole Mwenyekiti wa umoja wa walimu wakuu wa shule za msingi Tanzania Bara ameishukuru serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kulipa walimu mishahara yao kipindi chote shule zilipofungwa kutokana na ugonjwa wa Corana.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post