VIKAO VYA KAMATI ZA BUNGE KUANZA JANUARI 18


Vikao vya kamati za Bunge la Tanzania vinatarajiwa kuanza Januari 18 hadi 31, 2021 jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Januari 13, 2021 inaeleza kuwa shughuli zitakazofanywa ni pamoja na uchaguzi wa wenyeviti na makamu wenyeviti wa kamati.

Pia mafunzo kwa wajumbe wa kamati za kudumu kuhusu majukumu na taratibu za uendeshaji wa kila kamati na mafunzo kuhusu Bunge mtandao na usalama wa mitandao ya kamati zote.

Shughuli nyingine ni kamati za kisekta kupokea maelezo ya wizara kuhusu muundo, majukumu ya taasisi pamoja na sera na sheria zinazosimamiwa na wizara hiyo.

Nyingine ni mafunzo kwa kamati za Hesabu za Serikali (PAC), Kamati za Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati za Uwekezaji na Mitaji kwa Umma (PIC) na Kamati ya Bajeti.

Taarifa hiyo imesema mafunzo hayo yatahusu uchambuzi wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Msajili wa hazina (TR) na namna bora ya kuhoji maofisa masuhuli.

Nyingine ni mafunzo kwa Kamati ya Sheria Ndogo kuhusu uchambuzi wa sheria ndogo na uzoefu wa mabunge mengine ya nchi zinazofuata mfumo wa kibunge wa jumuiya ya madola.

Kwa upande wa kamati ya Bajeti, taarifa hiyo imesema watapokea tathimini ya utekelezaji wa mpango wa pili wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano wa 2016/2017 hadi 2020/2021.

Pia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/22 hadi 2025/26 na mwongozi wa kuandaa mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Shughuli nyingine ni utekelezaji wa bajeti ya Serikali pamoja na Sheria ya Fedha kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

 Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post