TAMISEMI KUSHIRIKIANA NA SHIRIKA LA AGRI THAMANI


Mhe Neema Lugangira (Mb) akiwasilisha Mada kwa Washiriki wa  Bukoba DC wakati wa utoaji wa elimu ya lishe bora wa shirika hilo kwa Viongozi wa makundi mbalimbali kama sehemu ya kuhakikisha malengo ya Lishe yaliyowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 yanatekelezwa.
Mwita Waibe, Mratibu wa Lishe OR TAMISEMI akisisitiza umuhimu wa Ajenda ya Lishe kwa Washiriki, Bukoba DC
Madiwani na Viongozi wa UWT wakifuatilia kwa karibu Mafunzo ya Lishe Bora


Mhe Neema Lugangira (Mb) akimpokea Mhe Murshid Ngeze, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini alipowasilini kwenye Mkutano. Mwenyekiti aliambatana na Afisa Lishe Wilaya aliyevaa shati yenye mistari

 

NA MWANDISHI WETU,BUKOBA

 

MRATIBU wa Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dodoma Mwita Waibe amesema watahakikisha wanashirikiana na Shirika la Agri Thamani ambalo limekuwa likitoa elimu ya umuhimu wa lishe bora na athari zake endapo hazitatiliwa mkazo ili kuweza kuibadilisha jamii husika.

 

Mwita aliyasema hayo wakati wa utoaji wa elimu ya lishe bora wa shirika hilo kwa Viongozi wa makundi mbalimbali kama sehemu ya kuhakikisha malengo ya Lishe yaliyowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 yanatekelezwa. 

 

 Alisema Ofisi ya Rais TAMISEMI imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Agri Thamani kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi huku akiwapongeza sana Agri Thamani kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya kuhakikisha elimu ya Lishe Bora inafika ngazi ya jamii ambapo ndio haswa kazi kubwa ilipo. 

 

Elimu hiyo ambayo imekuwa chachu kubwa imeweza kuwafikia madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mjini wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ambao wamenufaika na semina hiyo hususan katika vipengele vya mikataba ya lishe iliyosainiwa kuanzia ngazi ya mkoa hadi kijiji,

 

“Lakini pia bajeti za lishe na sasa malengo ambayo CCM imejiwekea kwenye Ilani ya Uchaguzi ambayo kimsingi wanajukumu la moja kwa moja kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa na mafanikio makubwa kwa jamiii husika”Alisema

 

AWALI Afisa Lishe wa Wilaya ya Bukoba Vijijini Desdery Karugaba,  amewashukuru Agri Thamani kwa kuandaa Semina hiyo ambayo sasa inakwenda kuongeza kasi  ya jitihada za kutokomeza udumavu na utapiamlo kwa ujumla wilayani hapo. 

 

“Kwa kweli niseme kwamba semina hii itakuwa chachu kubwa ya kuweza kuongeza jitihada za kutokomeza udumavu na utapiamlo kwa ujumla kwa wilayani hapo”Alisema

 

Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe Murshid Ngeze alisema kwamba wao kama Halmashauri wanaelekeza ajenda ya Lishe Bora iwe ya Vitendo na kuahidi matokeo yataonekana maana ni lazima kama Halmashauri wawe mstari wa mbele kuikoa rasilimali watu. 

 

Hata hivyo Mhe Mbunge Neema Lugangira ambaye pia ni Mkurugenzi wa Agri Thamani amesema kwa kuanzia semina hizi zimeshafanyika Dodoma na hivi sasa zinaendelea mkoani Kagera na zitafanyika Tanga na Kigoma.

 

"Dhamira yangu binafsi ni kuiona Ajenda ya Lishe inakuwa ajenda ya kila Mtanzania na kila mtu kwa nafasi yake anakuwa sehemu ya kuchangia kutokomeza udumavu kuanzia ngazi ya jamii inayotuzunguka", Mhe Neema Lugangira alimalizia


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments