Nguruwe
Na Josephine Charles
Manispaa ya Shinyanga imepiga marufuku kuingiza Nguruwe kutoka maeneo ambayo yameathirika na Homa ya Nguruwe ikiwemo Wilaya ya Kahama kutokana na homa hiyo kuzuka katika wilaya hiyo na kusababisha vifo vya nguruwe zaidi ya 500.
Marufuku hiyo imetolewa na Afisa Mifugo wa Manispaa ya Shinyanga, Chrispacy Kasimbazi wakati akizungumza katika kipindi cha Mambo Leo kinachorushwa na Radio Faraja Fm Stereo kila jumatatu hadi ijumaa saa tatu asubuhi hadi saba kamili mchana.
Amesema wafugaji wote wanatakiwa kufuata utaratibu wa malisho ya nguruwe,kuwa na vitendea kazi maalum wakati wa kuwahudumia wakiwa kwenye banda lao ili kuwaepusha na homa hiyo kwa kuwa inasababishwa na kirusi ambacho hata binadamu anaweza kukibeba kutoka kwa nguruwe ambaye tayari anavyo akaenda kumhudumia nguruwe mwingine na kumsababishia maambukizi ya kirusi hicho kinachosababisha Homa ya nguruwe isiyo na chanjo wala Tiba.
Aidha, Kasimbazi ameeleza kuwa ugonjwa huo unaenezwa kwa njia ya virusi na unaambukizwa kwa njia ya nguruwe wenyewe wakiwemo nguruwe pori kukutana na nguruwe wanaofugwa na binadamu, kwa njia ya kupe, chakula, kinyesi au maji maji ya mwili.
Ameeleza dalili za Homa ya Nguruwe kuwa ni rangi nyekundu kama vile kuvia damu kwenye masikio, kifua, mapajani na maeneo mengine ya mwili wa Nguruwe lakini mbali na dalili hizo homa ya Nguruwe haiwezi muathiri kiumbe mwingine aidha binadamu au wanyama wengine isipokuwa ni nguruwe wenyewe kwa wenyewe.
Afisa Mifugo huyo ameelekeza wafugaji wote wa nguruwe kuwa endapo wataona dalili zozote kama hizo alizotaja na nyinginezo watoe taarifa haraka sana kwa afisa mifugo wa kata yake au aliyekaribu naye ili wapate maelekezo sahihi ya kuwaepusha nguruwe wengine na homa hiyo.
Siku chache zilizopita serikali wilayani Kahama ilipiga marufuku biashara ya uuzaji na ulaji wa nyama ya nguruwe wilayani humo kutokana na kuibuka kwa homa ya nguruwe na kusababisha vifo vya nguruwe zaidi ya 500.